WAZIRI MKUU MAJALIWA APONGEZA HATUA ZA UFUTAJI WA LESENI NA MAOMBI YA LESENI YASIYO NA SIFA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim M. Majaliwa amepongeza hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Madini za ufutaji wa Leseni na kuondoa maombi yasiyo na sifa na kuitaka Wizara kuusimamia msimamo huo na kuyatenga maeneo kwa ajili ya wenye uhitaji wa maeneo ya uchimbaji hasa wachimbaji wadogo na wawekezaji walio tayari.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 27.06.2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma wakati akifunga maonesho ya wiki ya madini iliyoratibiwa na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA).

Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan imejizatiti kuhakikisha kwamba Sekta ya Madini inawezeshwa kibajeti ili kuchochea ukuaji wa shughuli za madini ili kuiwezesha sekta hii kutoa mchango unaostahiki kwa uchumi wa Tanzania na pato la Taifa ambapo kwa sasa mchango wa sekta kwa GDP umefikia 9%.

Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwapongeza wachimbaji wadogo nchini kwa mchango mkubwa wanaotoa katika kuchochea ukuaji wa uchumi nchini na kuzitaka Wizara za TAMISEMI na Madini kukaa pamoja kujadiliana na kutatua changamoto ya ongezeko la tozo za Halmashauri kwa wachimbaji wadogo.

Aidha,Waziri Mkuu Majaliwa amempongeza Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde kwa msimamo thabiti wa kufuta Leseni za utafiti ambazo hazifanyiwi kazi na kushikilia eneo kubwa hivyo kukosesha upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo.

Naye Waziri wa Madini,Mh. Anthony Mavunde amesema Wizara imejipanga kutekeleza maono ya kuhakikisha rasilimali madini inabadilisha uchumi wa nchi na kuwanufaisha watanzania.

Akitoa salamu za Bunge,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mh. Dkt. David Mathayo ameitaka serikali kuhakikisha inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo ili kuwaendeleza na kukua kutoka uchimbaji mdogo.

Naye Rais wa FEMATA,Ndg. John W. Bina ameiomba serikali kuondoa vikwazo vya kuingiza madini nchini kutoka nchi jirani ili kuchochea biashara ya madini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya Madini barani Afrika.

Post a Comment

Previous Post Next Post