Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza Taasisi za Umma nchini kuweka mikakati madhubuti ya matumizi ya mifumo ya kidigitali ili iweze kutumika kuboresha utendaji serikalini.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma na uzinduzi wa mifumo ya kidijitali iliyosanifiwa na wataalamu kutoka Tanzania yaliyofanyika tarehe 23/06/2024 katika viwanja vya chinangali jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Taasisi za serikali kuweka mipango madhubuti ya muda mrefu na mfupi ya jinsi mifumo hiyo ya kidijitali itakavyotumika kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
Maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yaliambatana na maonesho ya Taasisi za serikali yenye lengo la kutoa elimu kuhusu majukumu ya Taasisi hizo pamoja na kuongeza ushirikiano na ushirikishwaji kati ya serikali na sekta binafsi.
Mifumo iliyozinduliwa ni Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-WATUMISHI), Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi (PEPMIS kwa watumishi wa Umma na PIPMIS kwa taasisi za Umma), Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) na Mfumo wa e-Mrejesho. TCRA ni kati ya taasisi za umma zinazotumia mifumo tajwa kikamilifu na kuendelea kuboresha kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika shughuli zake ilikuakisi utumishi wa umma wenye ufanisi na uwajibikaji katika kufikia ustawi wa Taifa.
TCRA imeshiriki kwenye maonesho hayo kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni na kuwafikia wananchi waliopatiwa maelezo zaidi kuhusu sekta ya mawasiliano nchini.