MKOA WA KIMADINI CHUNYA WAKUSANYA ZAIDI YA BILIONI 30


Mkoa wa kimadini Chunya mpaka kufikia Juni 7, 2024 umefanikiwa kukusanya maduhuli ya Shilingi bilioni 34.9 katika mnyororo wa uchimbaji madini.

Hayo yamebainishwa leo Juni 7, 2024 na Afisa Madini Mkazi (RMO) mkoa wa kimadini  Chunya  Mha.Laurent Mayala  wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa sekta ya Madini wilayani Chunya kwa  Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali.

Mha.Mayala amesema kuwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 Ofisi imefanikiwa kudhibiti matukio ya utorosha madini ambapo mpaka sasa kiasi cha gramu 8,189.79 za madini ya dhahabu zimekamatwa.

Akielezea kuhusu mwenendo wa utoaji leseni za ununuzi mdogo na mkubwa wa madini , Mha.Mayala amesema kuwa , idadi ya leseni 65 zimetolewa kwa wanunuzi wakubwa wa madini na leseni 315 za wanunuzi wadogo.

Akifafanua juu ya kuwaendeleza wachimbaji  wadogo wilayani Chunya Mha.Mayala amesema kuwa tayari wametenga  maeneo  mbalimbali ikiwemo Makongolosi , Mawelo,Sagambi, Matundasi na Kasisi kwa ajili ya kurasimishwa kwa wachimbaji wadogo ili kukuza shughuli zao za uchimbaji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameipongeza Ofisi ya Madini Wilayani Chunya kwa kufanya vizuri katika usimamizi mzuri wa shughuli zote zinazohusiana na sekta ya madini.

Mahimbali ameongeza kuwa mkoa wa Kimadini Chunya ni mmoja wa mkoa muhimu sana katika sekta ya madini hivyo  amewaataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa  weledi , ushirikiano na kuongeza ubunifu ili kuendelea  kufikia malengo yaliyowekwa.

Ziara hii ya siku mbili wilayani Chunya Mahimbali ameambatana na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za uchimbaji , uzalisha na uchenjuaji  katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.

Post a Comment

Previous Post Next Post