MKANDARASI CRJE EAST AFRICA LTD ATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA KWA WAKATI


NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa Mhe. Zainab Katimba amemuagiza Mkandarasi M/s CRJE East Africa LTD kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara Wafipa - Kagera na Bangwe- Burega kwa wakati.

Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo Mei 31, 2024  wakati alipokagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata ya Bongwe, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.

Amemtaka Mkandarasi  kufuata sheria, taratibu na miongozo  iliyowekwa kwenye mikataba ambayo inaeleza wazi  barabara hiyo inatakiwa kukamilika  lini ili wananchi waweze kupata huduma za usafirishaji.

Wakandarasi mnapopatiwa kazi jukumu lenu ni kutekeleza kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa kwa kuwa mnapokuwa nyuma ya ratiba mnakwamisha maendeleo ya wananchi.

Amemtaka kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati kwa kuwa wananchi wanamatarajio makubwa na Serikali inahitaji kuona fedha inayotengwa kwa ajili ya ujenzi  inaleta matokeo chanya.

Aidha amesema Serikali haitafumbia macho ucheleweshaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara ama kusuasua kwa utekelezaji wa miradi nchini.

Naye Diwani wa Kata ya Bangwe Mhe. Hamis Besere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha  zaidi ya trioni 11 kwa ajili  utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo  mkoani Kigoma.

Aidha, amewaomba wakandarasi wanaojenga miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo kujenga kwa ubora unaotakiwa na kuikamilisha ndani ya muda wa makubaliano.

Post a Comment

Previous Post Next Post