Mkurugenzi wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume ameelekeza magari yote yaliyotolewa na serikali kwaajili ya Usimamizi wa shughuli za Afya kutumika kwa shughuli iliyokusudiwa badala waganga wakuu wa halmashauri kuyamiliki kwa shughuli zao.
Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo mkoani Songwe akiwa ameambatana na timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI wakati wa ziara ya usimamizi shirikishi na ukaguzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika Halmashauri za Mji Tunduma na Halmashauri ya Ileje zote za mkoa wa Songwe .
“Yale magari ambayo tumeyatoa ya usimamizi shrikishi sio magari ya waganga wakuu wa Halmashauri ni Magari ya CHMT(Timu za Usimamizi wa Shughuli za Afya za Halmashauri) hivyo yanatakiwa kwenda kufanya kazi za usimamizi shirikishi na maeneo ambayo tumepita tumeona hilo ‘gap’ kwa Tunduma tumepita katika kituo cha Afya tumeona mapungufu na kama timu zetu tungekuwa tunatembelea tukafanya ziara shirikishi mapungufu yasingeonekana”
Dkt. Mfaume amesisitiza kuwa uboreshaji wa Huduma za Afya unaendana na usimamizi shirikishi hivyo amezitaka timu za usimamizi wa shughuli za Afya za Halmashauri (CHMT) na Mkoa (RHMT) kutembelea mara kwa mara maeneo ya kutolea Huduma ili huduma zitolewe kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine Dkt. Mfaume ameelekeza matumizi ya mfumo wa kielekroniki ya taarifa mbalimbali kwenye maeneo yote ya kutolea Huduma za Afya iliyowekwa na serikali ikiwemo mfumo wa udhibiti wa taarifa za wagonjwa na Mapato (GoTHoMIS)
Kwa upande wake Mwanaisham Nassor, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Tunduma amekiri kuwepo kwa mapungufu hayo katika maeneo ya kutolea Huduma za Afya na ameahidi ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri kuanza kufuatilia kwa karibu ili wananchi wapate huduma stahiki.