BITEKO: BILA WAVUVI WADOGO HAKUNA UVUVI NCHINI


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini yanategemea wavuvi wadogo kwa sababu asilimia 95 ya shughuli za uvuvi zinafanywa na wavuvi wadogo.

Amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wavuvi Wadogo Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia leo Juni 5-7, 2024.

Dkt. Biteko amesema kufuatia umuhimu wao huo ndio maana serikali imefanya juhudi za kutosha katika kukuza uvuvi mdogo ikiwemo kuandaa na kutekeleza sera, sheria, kanuni, miongozo na mikakati mbalimbali ya kuendeleza miundombinu ya masoko na mialo, uanzishwaji wa dawati la sekta binafsi linalolenga kukuza uwekezaji kwenye uvuvi mdogo na kuwezesha wavuvi wadogo kupata mikopo yenye masharti nafuu kutoka katika taasisi za fedha.

Kupitia mkutano huo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wizara na wadau wengine kutoka nchi mbalimbali Afrika kutengeneza mifumo mizuri ya kuwawezesha wavuvi wadogo kuinua shughuli zao ikiwemo kuwawatafutia mitaji na masoko ya bidhaa zao.

Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa serikali itaendelea kuwawezesha wavuvi wadogo zana na pembejeo ikiwemo kutoa misamaha ya kodi ili kuwapunguzia mzigo wa uendeshaji wa shughuli zao huku akisisitiza kuwa ni  matarajio yake kwamba mkutano huo utatumika kubadilishana uzoefu, kuleta ufumbuzi wa changamoto na kupatikana kwa sauti ya pamoja ya kusemea uvuvi mdogo kwenye jumuiya za kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa ni heshima kwa nchi  ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kwanza barani Afrika kwa upande wa wavuvi wadogo huku akibainisha kuwa lengo la mkutano huo nikutoa fursa kwa wavuvi wadogo kushiriki na kupaza sauti zao juu ya kuboresha uvuvi mdogo ikiwa ni pamoja na kuwezeshwa ushirikishwaji kwenye michakato ya uundwaji na utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, mipango na mikakati yote inayohusu wavuvi hao.

Mkutano huo wa Uvuvi barani Afrika ni matokeo ya Mkutano wa Maadhimisho ya Mwaka wa kimataifa wa Wavuvi wadogo na wakuzaji Viumbe Maji (IYAFA) uliofanyika mwezi Machi, 2023 jiji la Rome nchini Italia.

Post a Comment

Previous Post Next Post