WANANCHI TUNZENI MIUNDOMBINU YA BARABARA - MHE. LONDO


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Tawala za  Mikoa na  Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa rai kwa  wananchi wa kata ya Minyughe na Makilawa kuhakikisha wanatunza miundombinu ya daraja la MInyughe lililojengwa  kwa gharama ya shilingi bilioni  1.8

Rai hiyo imetolewa na  Mwenyekiti wa Kamati  Mhe.Denis Londo  leo Mei 25,2024 wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya Wakala wa  barabara za Vijijini na Mijini  (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ,Mkoani Singida

Amesema ujenzi  wa daraja hilo la chuma lenye urefu wa mita 30 katika barabara  ya  Mtamaa- Minyughe hadi Mtavila yenye urefu wa km 27 itafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo

Mhe. Londo amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini hivyo ni wajibu wa kila mwansnchi kuhakikisha wanatunza miundombinu inayojengwa

"Kuna  baadhi ya wananchi wachache  ambao si waaminifu huaribu  miundombinu na wengine kuchukua kama vyuma chakavu hili halikubaliki kila mwananchi anawajibu wa kulinda miundombinu hiyo"amesisitiza

Naye Mbunge wa Singida  magharibi  Elibariki Kingu  ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita  chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya mendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida

Aidha, ameipongeza Serikali kwa ujenzi wa Daraja la Minyughe  ambalo limesaidia kupunguza kero kwa wananchi wa maeneo hayo hasa wakati wa kipindi cha  mvua

Post a Comment

Previous Post Next Post