Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amekutatana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya Mhe Victoria Mwanziva, Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Joseph Kamonga, Mwenyekiti CCM Wilaya Mzee Kolimba sambamba na mkandarasi wa NIPO Africa Marcus Gondwe.
Viongozi wa Wilaya ya Ludewa wamefika ofisi za Wizara ya Maji Dodoma kwa mualiko aliotoa kwao tarehe 05 Mei 2024 alipopata wasaa wa kuwasiliana kwa njia ya simu katika Jukwaa la Wadau la Maji.
Aidha Lengo la Kikao hiki nikusukuma na kufanikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa Maji wa mji wa Ludewa wenye kiasi cha shilingi Bilion 7.4 unaohusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu.
Kwa pamoja viongozi wameweka mikakati madhubuti ya kuukamilisha haraka Mradi huu kwani kukamilika kwake kutapelekea Ludewa mjini kupata maji kwa asilimia 95%.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso amewapongeza Viongozi wa Wilaya ya Ludewa kwa kuwa mstari wa mbele kupigania na kufuatilia maendeleo ya wananchi hususani huduma muhimu ya Maji.
