Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema serikali imeweka utaratibu kwa watu wanaojitolea katika ajira kupewa kipaumbele pale ajira zinapotoka.
Dkt. Mollel amebainisha hayo Bungeni leo Jijini Dodoma wakati akijibu swali Namba 436 la Mbunge wa Viti Maalum Mhe.Conchesta Leonce Rwamlaza aliyeuliza Je, ni kwa nini Kada zinazowezesha utendaji kazi katika Hospitali hazijumuishwi pindi ajira zinapotangazwa?
Dkt. Mollel amesema kwa sasa utaratibu wa ajira kwa kada ambazo ni saidizi mfano Wahasibu, Maafisa ugavi na Madereva unafanywa na sekretarieti ya ajira na Utumishi hivyo hazijumuishwi kwenye kada zawatumishi wa Afya kama Madaktari, Wauguzi na Wafamasia ambao utaratibu wa ajira husimamiwa na Wizara ya Afya.
“Ili kupunguza tatizo hili tutaboresha mkakati wa mawasiliano ndani ya Serikali kwa kuonesha mahitaji halisi ya kada hizo ili vibali vya ajira vinavyotolewa vizingatie pia mahitaji ya kada husika ndani ya Wizara ya Afya”, ameeleza Dkt. Mollel.
