SHAKA ATAKA IMANI ZA DINI ZIENDELEE KUWAUNGANISHA WATANZANIA


Mkuu wa Wilaya ya Kilosa  mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, amewashauri Watanzania kuutumia mwezi mtukufu  wa Ramadhan kama jukwaa la kuwaelimisha wananchi washike  kamba moja ya kudumisha upendo, umoja na maelewano. 

Shaka ameyasema hayo leo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati wa mashindano ya kuhifadhi Quraani walioshirikisha washiriki kutoka  mkoa wa Pwani na Iringa yaliofanyika katika viwanja vya msikiti Bomani Morogoro.

Amesema siku zote  imani za dini zimekuwa zikitumika  na kuwa kiungo kinachounganisha  watu, hivyo vibaki kuwa mwiko na marufu dini kutumika kuwagawa wananchi aidha kwa madhehebu zao, kanda au kwa makabila yao.

Shaka amesema kila mtanzania na muumini wa dini  yake aelewe kuwa taifa halina dini bali  wananchi  wake ndiyo wenye kufuata imani  za dini na viongozi wa dini wanatakiwa kulisimamia hilo.

"Kila mtanzania nchi yetu inamtambua ni binadamu anayestahili heshima na haki kwa mujibu wa katiba  yetu. Taifa  letu  katiba yake imempa uhuru  wa kuabudu bila kuvunja mpaka, Kikitokea chama au kundi  chenye lengo la kuvuruga amani na kupandikiza chuki lilaaniwe na jamii ya watanzania,"amesema Shaka na kuongeza kuwa;

"Tunahitaji kumshuhudia kila mwananchi akipanda mbegu za amani, umoja na upendo, tunamshukuru Mungu tunaye Rais, Samia Suluhu Hassan, mwenye hofu ya Mungu kazi kubwa anaiyoifanya kutuunganisha kama Taifa inahitaji kuungwa mkono na kila mmoja wetu ili kuchochea maendeleo endelevu ndani ya nchi"amesema Shaka.

Aidha, Shaka aliwataka viongozi  wa dini  waendelee na kazi ya kuipika mioyo  ya waumini  wao  huku wakiwahimiza na kuwaeleimisha fadhila na neema za kumuamini Mungu ili waifanye mioyo yao iwe na rutuba ya upendo na kuwajali wenye dini na hata  wasio na dini. 

"Nawahusia muufanye mwezi huu mtukufu  wa Ramadhan uwe jukwaa la uadilifu linalotoa elimu itakayowajengea maarifa  waumini  na wasio na dini .Viongozi  wa dini zote waendelee kuhubiri upendo ndani na nje ya nyumba za ibada. Misikiti na makanisa yaendelee na kazi ya kuelimisha imani na umoja,"

Amesema kila muumini  wa dini anahitaji kupata nafasi ya kumuabudu mola wake akiwa katika  mazingira ya amani na utulivu  kwani amani na umoja  vikitoweka husababisha vurugu na kushindwa kufanya ibada.

Naye kadhi wa mkoa wa Morogoro, Mohamed Masenga, amesifu jitihada za viongozi wa serikali katika kuwaunganisha watanzania jambo ambalo nchi imeendelea kuwa na amani, upendo na umoja huku wakishuhudi mipango mbali mbali ya kuletea maendeleo ikifanikiwa. 

Post a Comment

Previous Post Next Post