Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Mahawanga Janeth ameungana na Jukwaa la Wanawake Kata ya Mabwepande katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanamke Duniani kwa kuwasilisha zawadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni mashuka katika wodi ya wazazi hospitali ya Wilaya ya Kinondoni ( Mabwepande Hospital) sambamba na kutoa zawadi mbalimbali kwa akina mama waliojifungua katika wodi ya Wanawake.
Katika maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 08 mwezi wa tatu na kwa mwaka huu 2024 kauli mbiu ni "Wekeza kwa Wanawake kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii" Mh. Mahawanga ameungana na jopo kubwa la Wanawake wa Kata ya Mabwepande waliopo katika Jukwaa la Wanawake wa Kata hiyo sambamba na Viongozi kutoka Umoja wa Wanawake wa CCM ( UWT ) kwa kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mlezi wa Majukwaa yote kwa kutoa zawadi ya mashuka katika hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya nchini pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kuhakikisha kila Kata inakuwa na huduma bora za afya kwa ajili ya jamii.
Mh. Mahawanga ambaye ni mlezi wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Mabwepande amefurahishwa sana na namna ambavyo wamejipanga vyema katika kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kusaidia Wanawake wenzao kwenye maeneo tofauti ambapo amewaahidi kuendelea kuwa nao bega kwa bega kuhakikisha Jukwaa linakuwa zaidi na dhamira ya kumkwamua Mwanamke kiuchumi inafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Aidha Mhe. Mahawanga amewaomba pia Wanawake kutokata tamaa kwa kuendelea kushirikiana pamoja maana ushindi wa pamoja ni bora zaidi kuliko ushindi wa mtu mmoja mmoja hivyo kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema ameahidi naye kuwa chachu ya kutoa fursa kwa wanawake wenzake na kuwasaidia kupitia Serikali na wadau mbalimbali wa Maendeleo kwani kuwekeza kwa Wanawake ni sehemu sahihi ya kuleta mafanikio kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Naye Mganga Mfawidhi msaidizi wa Hospital ya Mabwepande Dkt. Marco Silas Mtaita amepokea zawadi hiyo ya Mashuka kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluh Hassan na kumuomba Mbunge wa Viti Maalum Mh. Mahawanga kufikisha salamu za shukrani kwa Rais kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele na balozi wa kweli kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma bora na ya uhakika ya Afya lakini pia namna ambavyo ameiwezesha Hospitali ya Mabwepande kitengo cha Wazazi kutoka kutoa huduma ya kuzalisha wamama 10 kwa njia ya kawaida mpaka 100 kwa mwezi kwa njia ya upasuaji kutoka wamama 5 mpaka kufikia idadi ya kuzalisha wamama 30 kwa mwezi.