
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itajenga kituo cha Askari Wanyapori katika kijiji cha Mushabaiguru kata ya Kihanga Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, ili kuzuia tembo na wanyamapori wengine wanaovamia makazi ya watu na kuharibu mazao.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba katika ziara yake kijijini hapo na kusema Serikali imeshatenga maeneo kwa ajili ya kujenga vituo na nyumba za askari wa wanyamapori ili waweze kuwa karibu na makazi hayo.
"Mheshimiwa Rais ametuagiza tuhakikishe tunatatua kero za wananchi na kuongeza vitendea kazi ili zoezi la kudhibiti wanyama wakali na waharibifu liweze kufanyika kwa ukamilifu zaidi, na sisi kama Wizara tutafanyia kazi kila changamoto itakayoonekana kwa kadri ya uwezo wetu", amesema Wakulyamba.
Aidha, Wakulyamba amesema Serikali imeanza kupitia vigezo na viwango vya ulipaji wa fidia na kifuta machozi kwa wananchi walioathirika na kuharibiwa mali zao kutokana na uvamizi wa wanyamapori ili viweze kuendana na hali na gharama za maisha ya sasa hivi.
Amesema uvamizi wa Wanyamapori kwenye makazi unachangiwa na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na kufanyika kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi.
Kwa Upande wake, Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe amesema miongoni mwa changamoto inayosababisha Wanyamapori hao kuvamia makazi ya wananchi wa Kihanga ni pamoja na upanuzi wa mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari cha Kagera (Kagera Sugar) ambapo wamechukua maeneo ya misitu na kufanya kilimo cha miwa katika Kata hiyo.
Naye, Diwani wa kata ya Kihanga Ndg. Steven Rwamuhangi amesema Wanyamapori wamekuwa ni changamoto kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Mushabaiguru na maeneo jirani kwa kusababisha vifo kwa wananchi pamoja na uharibifu mkubwa wa Mazao na Mashamba ya Wananchi.