AWESO APONGEZA MAJI KUJAA BWAWA LA UMEME LA NYERERE KABLA YA WAKATI ULIOPANGWA


Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa, Wizara ya Maji kupitia Bonde la Mto Rufiji na mabonde yote ya Maji chini ya usimamizi wa Wizara ya Maji ambayo yanatiririsha maji Bwawa la Mwalim Nyerere kupitia mikoa takribani 10 yemefanikisha Maji kupatikana ya kutosha kabla ya muda uliowekwa.
Ameeleza kuwa, ujazo wa maji unaohitajika katika Bwawa la umeme la JNHPP ni mita za ujazo bilioni 32.7 na sasa kuna mita za ujazo bilioni 28 hivyo bado mita nne tu Bwawa hilo kujaa kabisa.

Waziri Aweso amesema Mnamo tarehe 12 mwezi Disemba 2022 Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi zoezi la ujazaji wa maji katika bwawa la kufua umeme la Mwl. Nyerere. 
Matarajio ilikuwa ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwezi Juni 2024 maji yawe yamejaa na kufikia kiwango cha juu cha uzalishaji wa umeme ambao ni mita za ujazo bilioni 32.7. 

Aidha, Wizara ya Maji kupitia Bodi ya Maji Bonde la Rufiji ilipewa jukumu la kuhakikisha maji yanajaa kwa wakati. Mpaka kufikia leo maji yaliyopo kwenye bwawa yamefikia mita za ujazo bilioni 28. 
Hivyo basi, zimebaki mita za ujazo bilioni 4.7 tu ili bwawa liweze kujaa. Kulingana na takwimu zilizopo, kiasi cha maji kilichobaki kitakuwa kimejaa kabla ya tarehe 10 Mwezi Machi na hivyo kupelekea kuvuka matarajio ya kujaza bwawa Mwezi Juni. 

Katika hatua nyingine Waziri Aweso ametoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutofanya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji pia wasichepushe maji kiholela

Akisisitiza zaidi juu ya utunzaji wa vyanzo vya Maji , Aweso ametoa wito kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya Maji ambao ndio unasababisha mabwawa ya umeme kuwa na maji ya kutosheleza kuzalisha umeme na pia kutoa elimu kuhusu athari za kuharibu vyanzo vya maji vinavyopeleka maji pia katika mabwawa ya umeme.

Post a Comment

Previous Post Next Post