Waziri wa afya Ummy Mwalimu leo akipokea vifaa tiba amesema tunayo furaha kushiriki mafanikio katika kuboresha afya ya uzazi, mama, na mtoto nchini. Kulingana na Utafiti wa Demographia ya Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria 2022, vifo vya uzazi vimepungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, na vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000.
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejitolea kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa, ikilenga kufikia malengo endelevu ya Milenia 2030. Hatua zimechukuliwa, kama ujenzi wa vituo vya huduma za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC) kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi 523 mwaka 2023, na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya.
Pia, Serikali imeboresha huduma za afya ya uzazi kwa kujenga wodi za uangalizi maalumu za watoto wachanga, kununua vifaa tiba na dawa, na kuajiri watumishi wa afya. Upatikanaji wa vitanda vya kutolea huduma umeongezeka kutoka 84,162 mwaka 2021 hadi 104,687 mwaka 2023.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanikisha ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS 14,953,854,357, vitasambazwa katika majimbo yote 214. Vifaa hivi, pamoja na vitanda, magodoro, mashuka, na meza za vitanda, vitaimarisha huduma za afya ya uzazi.
Tunashukuru wananchi kwa kutoa taarifa kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika huduma za afya. Kupitia simu ya bure 199 au mitandao ya kijamii ya Wizara, tunahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa, na Serikali itaendelea kutafuta ufumbuzi.
Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama, na mtoto. Tunaahidi kuendelea kumuunga mkono katika kuboresha zaidi huduma hizi. Tunawashukuru pia wadau wote kwa ushirikiano wao na serikali katika kutoa na kuboresha huduma ya afya ya uzazi mama na mtoto. Ushirikiano huu ni muhimu katika kufanikisha malengo yetu ya afya.