TARURA KUIENDELEZA TEKNOLOJIA YA UJENZI WA MADARAJA YA MAWE


Wakala ya Barabara za Vijiiini na Mijini (TARURA)  imejipanga kuiendeleza teknolojia ya ujenzi wa madaraja ya mawe nchini kwa lengo la kupunguza gharama za ujenzi.

Akiongea wakati wa hafla ya kumalizika kwa mradi wa Enabel ambao ni mfadhili mkuu katika ujenzi wa madaraja hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi  Edward Amboka amesema licha ya kuwa mradi huo umefika mwisho tayari wahandisi wengi nchini pamoja na mafundi wanaelewa namna ya kujenga madaraja  ya mawe. 

"Teknolojia hii ni muhimu sana kwetu kwani inawezesha kutekeleza miradi kwa gharama nafuu na mpango wa TARURA  nikuhakikisha nchi nzima hasa maeneo yenye fursa ya mawe teknolojia  hii inatumika ili tuweze kuifungua nchi kwa urahisi".

Akisoma taarifa ya ujenzi wa madaraja hayo kwa Mkoa wa Dodoma, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya  Dodoma Mhandisi Kasongo Morijo amesema kuwa madaraja ya mawe yanaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali mkoani humo likiwemo Daraja la midomo minne  lililopo eneo la Ng'ong'ona ambalo hadi kukamilika litagharimu shilingi milioni  110.5 na kama lingejengwa kwa zege lingegharimu shilingi milioni 312.2.

Wakala ya Barabara za Vijiiini na Mijini (TARURA) inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kama VETA na Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kuandaa wataalam na kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja ya mawe.

Post a Comment

Previous Post Next Post