MAVUNDE ACHANGIA SARUJI MIFUKO 500 UJENZI WA MADARASA NA MATUNDU YA VYOO DODOMA JIJI


Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo amekabidhi mifuko 500 ya saruji kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndg. John Kayombo kwa dhumuni la kuchochea ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo kwa shule za Msingi na Sekondari Dodoma Jiji.

Mavunde amekabidhi mifuko hiyo 500 leo Jijini Dodoma  na kutoa rai kwa wadau kuiunga mkono serikali katika kuboresha na kuiendeleza sekta ya Elimu Dodoma.

“Tunaishukuru serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya ujenzi wa madarasa inayoendelea Jijini Dodoma.

Katika mwaka huu wa fedha tunashuhudia miradi mingi mikubwa ya ujenzi wa Shule mpya za Msingi na Sekondari ndani ya kipindi kifupi sana.

Katika kuunga mkono jitihada za serikali,mimi pamoja na wananchi tumekuwa tukianzisha ujenzi wa madarasa wa shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuboresha sekta ya Elimu Jijini Dodoma.

Katika kuendelea kuchochea shughuli za maendeleo kwenye sekta ya Elimu nimechangia mifuko 500 ya saruji ili iendeleze ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Jiji”Alisema Mavunde

Akishukuru kwa mchango huo,Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndg. John L. Kayombo amemshukuru Mbunge  Mavunde kwa mchango wa saruji wenye thamani ya Tsh 9,000,000 na kwa kuwa mstari wa mbele katika shughuli za maendeleo na hasa sekta ya Elimu na kuahidi kuisimamia mifuko hiyo ili ifanye kazi iliyokusudiwa ya ujenzi wa madarasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post