Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Mahawanga Janeth amejumuika na Vijana zaidi ya 1,300 kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kwenye Kongamani kubwa la Biashara na Uchumi la “Jipange University Tour 2023” kama Mama ambaye wajibu wake pia ni kukaa na Watoto wake wa Vyuoni na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kuwajenga na kuwaandaa baada ya kuhitimu masomo yao hasa katika kuzipambania ndoto zao na kuona fursa zinazowazunguka.
Katika Kongamano hilo Mhe. Mahawanga ameupongeza Uongozi wa Taasisi ya WBM kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu na lengo lake mahususi la kuwakutanisha Vijana kutoka Vyuo Vikuu pamoja na kuzungumzia fursa mbalimbali zilizopo nchini kwa ajili yao hasa katika kuwaandaa kabla ya kumaliza masomo yao. Katika Kongamano hilo kulikuwa na mada zenye mashiko kutoka kwa Vijana nguli katika masuala ya kilimo, Ujasiriamali na Uchumi ambao wamejiajiri baada ya kumaliza Vyuo na wanafanya vizuri sana na wamefanikiwa kutengeneza ajira kwa Vijana wenzao.
Mhe. Mahawanga ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini kundi la Vijana lakini pia kwa mchango mkubwa kwa Vijana wa Tanzania kwani imeendelea kutoa fursa kwenye makundi mbalimbali ya Vijana kuanzia Vijana wa Mashuleni, Vyuoni, Wajasiriamali, upande wa Kilimo, Teknolojia, Mazingira. Sanaa na Utalii.
Mhe. Mahawanga pia amewasihi Vijana kuhakikisha wanajitafuta sasa hivi wakiwa Vyuoni ili wajipate na waone wanapenda nini na ndoto zao kuwa akina nani huko baadae. Mkoa wa Dar es Salaam una Vijana wengi ambao wanafanya vizuri sana kwenye kila sekta hivyo inakuwa rahisi kuwaunganisha nao ili baada ya masomo yao wapate mwanga wa kujua pa kuanzia.
Mwisho Mhe. Mahawanga amewaasa Vijana wajitahidi na wahakikishe wanaitumia vizuri elimu yao kwa manufaa ya Taifa, Familia na Vijana wenzao huko mitaani ambao hawakufanikiwa kufika Vyuo Vikuu. Wahakikishe wakati wa likizo wawe na utamaduni wa kujichanganya na wenzao ambao wapo kwenye shughuli za Ujasiriamali kwani wao kwa elimu waliyonayo wanaupeo na jicho linaloona mbali katika kuiangalia fursa lakini wenzao wanauelewa mpana wa shughuli za Ujasiriamali na Masoko hivyo wakishirikiana watafanya vizuri sana.
Na mwisho Mhe. Mahawanga amewahakikishia Vijana kuwa nao bega kwa bega katika safari yao ya kupambania ndoto zao, na amewaahidi kutowaacha nyuma.