Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema tume ipo katika mchakato wa maandalizi ya Dira mpya itakayo toa mwelekeo wa wapi nchi itakwenda miaka ijayo na mambo gani nchi inapaswa kuangalia.
Mafuru amesema hayo leo Disemba 1, 2023 wakati wa Mkutano wa Waandishi wa Habari na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo leo Disemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam.
“Tupo kwenye utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 ambayo imebakiza miaka miwili kufikia mwisho, kama serikali hatuwezi kukaa kusubiri mpaka ifike mwisho ndio tuanze maandalizi ya dira nyingine, tayari mchakato wa maandalizi ya dira mpya itakayo toa mwelekeo wa wapi nchi yetu itakwenda miaka ijayo, mambo gani tunapaswa kuyaangalia tayari mchakato huo umeanza, na mara tu itakapo kamilika hii dira tunayotekeleza sasa tutaanza utekelezaji wa dira mpya,” amesema Mafuru.
Amesema kuwa dira hiyo itakuwa ya tofauti kwa sababu ya mazingira ambayo nchi imekuwa ikitekeleza dira ya 2025 na mazingira yanayokuja huko mbele yamebadilika sana, lakini pia mazingira ya mbele yanaoneka yanabadilika kwa kasi zaidi kuliko mazingira yanayotekeleza sasa.
Aidha, amewataka Watanzania kwa pamoja kubangua bongo zao, na wakati watakapotakiwa kutoa maoni kuhusu mustakabali wa Taifa waweze kushiriki kikamilifu.
Tags
Habari