BALOZI KINGU ATOA WITO KWA VIONGOZI NA JESHI LA POLISI KUDHIBITI HUJUMA MIRADI YA NISHATI VIJIJINI


Viongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)  wametoa wito kwa  Viongozi wa Serikali za Mitaa na Jeshi la Polisi nchini kuongeza ulinzi kwenye Miradi ya umeme inayojengwa kwa ajili ya kufikisha huduma hiyo vijiji mbalimbali nchini.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu baada ya kutembelea ili kujionea utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu (Mzunguko wa Pili) mkoa wa Pwani huku  mkandarasi akieleza kupata hasara ya shilingi milioni 40 tangu kuanza kwa utekelezwaji wa mradi huo ndani ya mkoa huo kutokana hujuma pamoja na wizi wa vifaa mbalimbali.

Hasara hiyo inatokana na baadhi ya watu wasio na nia njema kuhujumu Miradi hiyo kwa kuiba vifaa kama nyaya, kuchoma moto nguzo pamoja na kuiba mafuta ya mashineumba (Transfomer).

Miradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2021 mkoani hapo ukiwa na thamani ya shilingi bilioni 40 ambapo jumla ya vijiji 402 vimefikishwa huduma ya umeme kati 417 vilivyopo kwenye mkoa huo huku vijiji vilivyobakia ni 15 ambapo jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha vinafikiwa na umeme kabla ya Mwezi Juni, 2024.

Akizungumza baada ya kutembelea Mradi huo wilaya ya Mkuranga, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati ya Vijijini (REB) Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu ameiziomba Mamlaka za Serikali kuweka nguvu kwenye eneo hilo ili kulinda miundombinu hiyo inayogharimu fedha nyingi.

"Miradi ina maslahi mapana kwa Wananchi hususan wa vijijini kwa sababu nishati ni kila kitu inawasaidia kwenye huduma za kijamii, vituo vya shule, vituo vya afya lakini pia kwa ajili ya kuchochea shughuli zao za kiuchumi," amesema Balozi Kingu.

Balozi Kingu amesema  wizi wa vifaa ikiwemo nyaya na kuchomwa kwa nguzo za umeme si wa kufumbia macho  huku akiomba Viongozi wa Serikali za ikiwemo Serikali za Mitaa na Jeshi la Polisi kusaidia.

"Wananchi ambao ni wafaidika wa Miradi tunaomba na wenyewe wajitahidi kuongeza nguvu ya kupambana na wahalifu na wakishindwa watoe taarifa," amesema

Amesema miradi hiyo inatija kubwa ikiwemo kuongeza fursa za ajira kwa vijana kujiajiri na kuongeza masuala ya kiusalama huku akieleza kuweka kuharibu miundombinu hiyo iliyojengwa kwa gharama kubwa ni hasara.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa (REA) Mhandisi, Hassan Saidy amesema ni muhimu Wananchi kuitunza miundombinu hiyo kwani ipo katika mikoa 25 Tanzania Bara ukitoa mkoa wa Dar es Salaam.

"Wale wanaoandaa mashamba wahakikishe wanakuwa waangalifu wasichome moto nguzo lakini unaweza kuona nguzo imelalia laini toa taarifa ili mkandarasi aje kufanya marekebisho," amesema 

Amesema kasi ya Wananchi kujitokeza kuunganishwa na huduma ya umeme wa REA kwa baadhi ya vijiji bado ni ndogo huku akieleza kila kijiji kinacho ingiziwa wananchi 66 wanaunganishwa kwa bei ya Shilingi 27,000 baada ya Serikali kulipa gharama nyingine.

"Lakini katika kijiji hiki cha Kikoo hapa Mkuranga ni Wananchi 20 tu wamejitokeza kulipa kiasi hicho cha kuunganishwa, natoa rai kwa Wananchi wengine kujitokeza kulipia ili waunganishiwe kwani wakandarasi wakitoka fursa hiyo haitakuwepo tena," amesema 

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally amesema mahitaji ya umeme katika wilaya hiyo yamekuwa yakiongezeka kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa.

"Wawekezaji wa viwanda wapo 248 lakini  viwanda vikubwa  wapo109, wilaya ina vijiji 125, kuna vijiji vichache havijafikiwa na huduma kutokana na changamoto ya kufikika kimiundombinu hususani visiwani," amesema 

"Serikali tunampango wa kuinua shughuli za  utalii katika visiwa vile na tuko kwenye hatua mbalimbali kualika taasisi zingine ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kupata kiwanja tuweze kufungua fursa," amesema 

Post a Comment

Previous Post Next Post