Waziri wa ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha kuwa Wakandarasi wasumbufu na wababaishaji hawapewi kazi za ujenzi wa barabara nchini kote.
Akizungumza alipokagua Barabara ya Handeni - Mafuleta yenye kilometa 20, Bashungwa amesema ni aibu kuwa na mkandarasi msumbufu anaechelewesha kazi na bado kupewa miradi mingine hali inachelewesha maendeleo kwa wananchi.
"Mtendaji Mkuu nakuagiza kuhakikisha Mkandarasi huyu HHEG hapewi mradi mwingine wa km 30 mpaka nitakapojiridhisha na kasi yake ya ujenzi wa km 20 alizonazo sasa ifikapo Januari mwakani " amesema Bashungwa.
Amemtaka Mtendaji Mkuu wa TANROADS kujipanga vizuri na kusimamia wataalam wake ili Barabara ziweze kukamilika kwa wakati
Aidha, Bashungwa amezungumzia umuhimu wa wakandarasi kuwa na uhusiano mzuri na wananchi katika ni maeneo wanayofanyia kazi kwani kufanya hivyo ni sehemu ya ulinzi kwenye miradi wanayoitekeleza.
Amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Tanga Eng. Eliazari Rweikiza kuhakikisha HHEG anayejenga Barabara ya Handeni-Mafuleta anaboresha barabara inayotumika kati ya Handeni na Kilindi ili kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi.
Bashungwa amamuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuhakikisha katika vipaumbele vyake vya barabara zitakazojengwa kwa lami iwe ni pamoja na barabara za Handeni-Mziha -Turiani( KM 108.2), Kiberashi-Songe (KM 33.5)na Songe-Gairo ili kuufungua vizuri mkoa wa Tanga hususan wilaya za Handeni na Kilindi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohammed Besta amesema tayari TANROADS imeshawapanga mameneja wa miradi katika miradi yote 69 inayoendelea nchini.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Handeni mjini, Ruben Kwagirwa amepongeza Serikali kwa ujenzi kwa miradi mbalimbali ya barabara inayoendelea mkoani Tanga na kusisitiza kwamba kufunguka kwa barabara ya Mkata -Kwamsisi (Km 36), Handeni Turiani (KM 108.2), Handeni- Kiberashi- Singida, (KM434), Kiberashi- Songe ( KM 33.5) na Songe -Gairo kutaufungua vizuri mkoa wa Tanga na kuuunganisha na makao makuu ya nchi Dodoma kwa njia fupi.
Waziri Bashungwa yupo katika ziara ya kukagua athari za mvua za vuli mkoani Tanga na kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja inayoendelea mkoani Tanga.
"WANANCHI ONDOENI HOFU DARAJA LA KIMANGE - PWANI HALIJAVUNJIKA BARABARA INAPITIKA"
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani imetolea ufafanuzi taarifa zinazosambaa mitandaoni kwamba daraja la Kimange lilipo Mkoa wa Pwani Barabara kuu ya Pwani – Tanga limekatika kutokana na mvua kubwa zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali hapa Nchini.
Akitoa taarifa kwa Umma leo tarehe 23 novemba 2023 baada ya kufika na kukagua daraja hilo; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka J. Mwambage amesema tangu juzi, jana na leo kuna taarifa zinapipitishwa kwenye mitandao ya kijamii zikihabarisha Umma kwamba eneo hilo ni hatarishi kwani daraja hilo limekatika.
Amesema ukweli ni kwamba daraja hilo ni salama magari yanaendelea kupita na hakuna tatizo lolote “mvua inanyesha tupo hapa hali ni salama kabisa watu waendelee kufanya shughuli zao za usafiri na usafirishaji bila kuwa na wasiwasi wowote ule, TANROADS tunawasihi Wananchi waendelee kutupa taarifa za kweli pale ambapo wanaona kumetokea changamoto ya kukatika kwa miundombinu ya barabara hasa kipindi hiki cha mvua kubwa’’.
Hata hivyo mnano tarehe 15/04/2023 zaidi ya miezi 7 iliyopita daraja hilo la Kimange lilipata hitilafu kwa maji kupita juu na kumomonyoa sehemu ya daraja na hivyo kulifanya lipitike nusu, Ofisi ya Meneja ya Mkoa wa Pwani ilifanya kazi kwa siku mbili na kurejesha mawasiliano na kwamba hata wakati huo ilipotokea hitilafu hiyo magari yaliendelea kupita kwa kupokezana kutoka upande wa Dar- es Salaam na Mkoa wa Tanga.
Tags
Habari