Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza ujenzi wa shule zote za wasichana za kitaifa za mikoa ukamilike ifikapo Desemba 2023 ili zianze kutumiwa na wanafunzi Januari, 2024.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri Mchengerwa leo mara baada kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Rukwa inayojengwa Laela katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kupitia mradi wa SEQUIP.
Amesema majengo yote ya shule za mikoa za wasichana yanatakiwa kukamilika kwa muda huo ili wanafunzi waliopangiwa katika shule hizo waanze masomo wakiwa katika miundombinu bora ya elimu.
Dkt. Msonde ameagiza shule hiyo ya wasichana ya Mkoa wa Rukwa ikamilike kwa wakati kwa kuwa ipo nyuma kwenye ujenzi ikilinganishwa na za mikoa mingine.
"Serikali haitaki kusikia habari ya kutokamilika kwa ujenzi wa shule ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa sh.bilioni tatu ijengwe, kitendo hichi kinaashiria kumkosea na kumuangusha katika utekelezaji wa nia yake ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini,"amesema.