Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Mkandarasi atakayetekeleza Ujenzi kwa Kiwango cha lami barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki (km 133.28), sehemu ya Bigwa – Mvuha (km 78) ameshapatikana na Serikali ipo katika hatua za Mwisho za kusaini Mkataba wa Ujenzi wa sehemu hiyo ya barabara.
Bashungwa ameeleza hayo kwa njia ya simu wakati akizungumza na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Mhe. Hamis Taletale, wakati alipoombwa kutoa ufafanuzi kwa wananchi wa kata ya Mkuyuni wilayani Morogoro Vijijini kuhusu ujenzi wa barabara hiyo.
“Barabara hii itajengwa na Mkandarasi China Railway 15 bureau group corporation, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa km 78 kuanzia Bigwa umeshakamilika, sasa hivi tupo kwenye hatua za mwisho za kusaini mkataba wa kuanza kujenga kwa Kiwango cha lami” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa mara baada ya taratibu za kusaini mkataba kukamilika, ataambatana na Mbunge huyo Taletale kufika jimboni hapo kumtambulisha Mkandarasi na kumkabidhi kwa Wananchi kwa aijli ya kuanza utekelezaji.
Ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu anapambana kiła siku kuhakikisha analeta maendeleo kwa Watanzania.
Nae, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki Mhe. Hamis Taletale amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.