Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu leo tarehe 22/11/2023 amefikisha kwa Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa kilio cha Wakazi wa Tanga Mjini hususani wa Kata ya Tangasisi kuhusu ujenzi wa Barabara ya Tanga Pangani ambao umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu na hivyo kuleta kero kubwa kwa wakazi wa Tanga wanaotumia barabara hiyo. Aidha Mhe Ummy amewasilisha kwa Waziri Bashungwa kilio cha fidia kwa wakazi wa Kata ya Tangasisi na Kata nyingine 8 waliobomolewa nyumba zao ili kupisha ujenzi wa barabara ya Tanga hadi Pangani. Mhe Ummy amewasilisha kero hizo kwa Waziri Bashungwa katika Mkutano wa hadhara wa kuelezea Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kata ya Tangasisi.
Akijibu kero hizo, Waziri Bashungwa alikiri kuwa ni kweli barabara hiyo ipo katika hali mbaya na hivyo wakazi wa Tanga wana haki ya kuilalamikia. Waziri Bashungwa amemtaka Mkandarasi wa barabara hiyo asiondoke site. Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan italeta mara moja shilingi bilioni 5 ili kuendeleza ujenzi wa barabara hiyo na kukamilika kwa wakati. Vilevile Waziri Bashungwa amelipokea suala la fidia na kuahidi kuendelea kulifanyia kazi.
Mhe Ummy na Diwani wa Kata ya Tangasisi Mhe Ahmed Mwinjanga walieleza miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kata hiyo chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambayo ni pamoja na;- ujenzi wa madarasa na maabara mpya shule ya Sekondari Japan, Ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Msingi Mwang'ombe, Ujenzi wa majengo mapya manne ya Kituo cha Afya Mwakidila pamoja na kukarabati na kufungua barabara mbalimbali za ndani katika mitaa ya kata ya Tangasisi.
Mkutano huu ulioandaliwa na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tanga chini ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya Meja Mstaafu Hamisi Mkoba pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya Ndugu Urasa Nanyaro, Waheshimiwa Madiwani, wajumbe wa kamati ya siasa Kata ya TangaSisi, viongozi na wananchi wa TangaSisi na kata za Jirani za Tanga Mjini.
Kabla ya Mkutano huu Mhe Ummy alishiriki kikao cha halmashauri kuu ya Ccm kata ya Tangasisi.
Tags
Habari