Mbunge wa Tanga Mjini Mhe Ummy Mwalimu ameanzisha Ligi ya Vijana ya Mpira wa Miguu inayojulikana kama Odo Ummy Cup Ligi hiyo itaanza kutimua vumbi Jijini Tanga tarehe 02/12/2023.
Ligi hii itajumuisha timu za Vijana kutoka kata zote 27 za Jiji la Tanga pamoja na Timu maalumu ya Hamasa ya UVCCM Wilaya ya Tanga. Ligi hiyo itachezwa kwa mfumo wa makundi katika Tarafa zote 4 za Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu zote 28 leo tarehe 26 Novemba 2023, Mhe Ummy ameeleza kuwa lengo la Ligi hiyo ni kujenga umoja na mshikamano baina ya Vijana wa Tanga Mjini, kulinda na kuimarisha afya za Vijana sambamba na kuibua vipaji vipya vya mpira wa miguu kwa Vijana wa Tanga Mjini. Kila timu leo imekabidhiwa seti 1 ya jezi na mpira 1.
Mwenyekiti wa Kamati ya Odo Ummy Cup ndugu Abdallah Saady Mapikipiki amesema kuwa Mshindi wa kwanza wa Ligi hiyo atapatiwa zawadi ya shilingi milioni 3; kikombe, jezi na mipira miwili. Mshindi wa Pili atanyakua shilingi milioni 2, ngao, jezi 1 na mpira 1 na Mshindi wa 3 atapata shilingi 1 atapata shilingi milioni 1. Ametoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipija vya vijana wa Tanga Mjini. Nae Mratibu wa Odo Ummy Cup, Ndugu Ibrahimu Kidiwa amewataka washiriki wa Ligi hii kuzingatia Sheria, Kanuni na Nidhamu za Mchezo wa Mpira wa Miguu.