WAZIRI MAVUNDE AMALIZA MGOGORO WA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI MAFURUNGU


Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amemaliza mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini uliodumu kwa mwaka mmoja katika Kitongoji cha Mafurungu ,Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Akizungumza katika Mkutano na wachimbaji wadogo hao,Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika ukuaji wa uchumi wa taifa hivyo inafanya kila juhudi ili kuona wachimbaji wadogo wa madini wapo katika mazingira salama ya uchimbaji.

Mhe.Mavunde amefafanua kuwa maana ya mazingira bora ya uchimbaji ni pamoja usalama katika uchimbaji, kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa lakini pia kuwa na taarifa sahihi za uwepo wa madini ili kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Mavunde ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wenu katika sekta ya madini leo tunafunga rasmi mgogoro kwa kuwapatia leseni nne za uchimbaji ili kila mmoja achimbe bila kuwepo na mgogoro wowote katika kitongoji cha Mafurungu.

Sambamba na hapo Mhe.Mavunde ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji katika maeneo yao ya kazi ambapo katika juhudi za kuunga mkono maendeleo ya kitongoji cha Mafurungu tayari ametoa ahadi ya mifuko 200 ya Saruji na kuwa Balozi wa kujitolea kwa eneo hilo.

Naye, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahm Mwanga ameupongeza uongozi wa Wachimbaji Wadogo wa madini kupitia Chama Cha Wachimbaji Wadogo Mafurungu (UWAWAMA) kwa kukubali na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Madini na kuweza kufuta sintofahamu zote zilizokuwepo awali.

Mbunge wa Jimbo la Mtera Mh. Livingstone Lusinde ameishukuru Serikali kupitia Waziri Mavunde kwa utatuzi wa mgogoro huu na kuwataka wachimbaji hao kuongeza uzalishaji zaidi ili kuinua mapato ya Halmashauri na serikali kuu kwa kuwa sasa wanachimba katika eneo rasmi tofauti na awali.

Awali , Meneja Mgodi Ndg.Mbwana Mosses akisoma taarifa ya mafanikio ya Chama chaUWAWAMA kuhusu uzalishaji wa dhahabu amesema kuwa hadi sasa chama kupitia migodi yake kimeweza kuzalisha kiasi cha gramu 11093.19 za dhahabu ambazo zina thamani ya TZS. 1,331,419,080.67 na kulipa Mrabaha wa TZS. 79,888,144.75.

Mkutano ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Chamwino, Afisa Madini Mkazi Dodoma,Viongozi wa Dini na wachimbaji wadogo madini.

Post a Comment

Previous Post Next Post