Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amegawa vifaa vya michezo kwa Timu zilizotinga 16 bora ya mashindano ya Dodoma Ndondo Cup 2023.
Mashindano ya Ndondo Cup Dodoma ni kati ya mashindano makubwa kuwahi kufanyika mkoani Dodoma yanayohusisha Timu kutoka kata mbalimbali za Dodoma Mjini.
Akizungumza katika hafla hiyo,Mbunge Mavunde ameendelea kusisitiza kwamba msingi wa mashindano hayo ni kutengeneza daraja la mafanikio kwa Vijana wanamichezo wa Dodoma Mjini ili kutumia vipaji vyao kujiendeleza kimaisha na kukua kiuchumi.
Mavunde ameeleza pia kwamba kusudio kubwa kwa sasa la mashindano haya ni kuyafanya kuwa eneo sahihi la kuibua na kuendeleza vipaji.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma(DOREFA) Ndg. Mohamed Aden amempongeza Mbunge Mavunde kwa jitihada kubwa ya kuwainua vijana wa Dodoma kupitia michezo na kuahidi kwamba DOREFA itakuwa naye bega kwa bega katika kuendeleza na kukuza michezo mkoani Dodoma.
Akizungumza awali,Mratibu wa Ndondo Cup Dodoma 2023 Ndg. Yahaya Mohamed (Mkazuzu) amezitaka timu zote kuhakikisha zinaheshimu na kufuata kanuni za uendeshaji wa Mashindano hayo ili kujenga usawa na haki.
