Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim M. Majaliwa amekutana na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari ya Posco Holdings, Posco International,SK, Korea Zinc na LX International kupitia madini ya kimkakati(_critical minerals_).
Waziri Mkuu Majaliwa amewaeleza wawekezaji hao juu ya utayari wa serikali katika kushirikiana nao katika uwekezaji wao kwa kuweka mazingira mazuri ya kisera na kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa njia ya barabara,maji,reli na anga.
Aidha Waziri Mkuu alipongeza hatua iliyofikiwa kwa kampuni tatu za FARU GRAPHITE CORPORATION, BLACK ROCK MINING LIMITED na POSCO INTERNATIONAL ya Korea Kusini kusaini Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding - MoU) kwa ajili ya mashirikiano ya kibiashara yatakayowezesha kampuni ya POSCO INTERNATIONAL kupata madini ya kinywe (_offtake deal_) kutoka Mradi wa kinywe wa Mahenge,Morogoro.
Akitoa maelezo ya awali,Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema ushirikiano wa Korea Kusini na Tanzania katika eneo hili la madini ya kimkakati litasaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa na kuongeza pia wamezungumza mazungumzo ya awali na wawekezaji hao juu ya kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pamoja na umuhimu wa kuongeza thamani ya madini hayo hapa hapa chini ili kuongeza tija na kuchochea uchumi wa ndani sambamba na upatikanaji wa ajira za kutosha kwa watanzania.
Mkuu wa Msafara wa Wawekezaji kutoka Korea Kusini Mh. Yoon, Sang Jick, Waziri Mstaafu wa Biashara, Viwanda na Nishati na Mjumbe Maalum wa Rais amesema ni dhamira ya Korea Kusini kuhakikisha inashirikiana na Tanzania katika eneo hili la madini mkakati na ndio sababu ameongozana na Kampuni kubwa za Madini na zenye uwezo mkubwa wa Mtaji na anaamini kupitia ushirikiano huu na milango iliyofunguliwa na serikali ya Tanzania wapo tayari kuleta uwekezaji mkubwa kwenye sekta hii ya madini na kusaidia kuikuza sekta hii.
Akitoa maelezo ya awali Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini Balozi Togolan Edris Mavula amesema ni fursa ya kipekee ya nchi ya Tanzania kulitumia vizuri soko la Korea Kusini kwa madini ya kimkakati na kwamba ubalozi wa Tanzania utaendelea kuratibu upatikanaji wa wawekezaji wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya sekta ya madini.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Madini Ndg. Kheri Mahimbali na wataalamu mbalimbali kutoka Taasisi za STAMICO,GST na Tume ya Madini.