Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kuacha tabia ya kukaa maofisini badala yake waende kuwahudumia wananchi kwa weledi.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo leo wakati wa Mkutano Mkuu wa Maafisa Ustawi wa Jamii uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Dotto Biteko kwa niaba ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango uliofanyika katika Ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.
“Wengi wenu mnafanya kazi kwa mazoea na mnakaa ofisini wakati jamii inawahitaji katika kutatua changamoto zao za masuala ya kijamii,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais-TAMISEMI haitosita kuwachukulia hatua maafisa wazembe na wasio waadilifu ambao wanakwamisha kesi za unyanyasaji wa kijinsia kwa kushawishi waathirika wasiende polisi kutoa taarifa za vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Sanjari na hilo, amewataka wakatoe elimu kuhusu athari za madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya makuzi ya awali ya mtoto ili kujenga taifa imara linalozingatia mila na desturi za kitanzania.
Mkutano huu wa siku mbili unajumuisha maafisa ustawi wa jamii wa mikoa na wilaya, wadau na watendaji wa wizara za kisekta ambao wamepata fursa ya kujadili masuala ya ustawi wa jamii ili kuboresha huduma kwa wananchi.