Serikali yabainisha kuwa ifikapo mwaka 2026/2027 korosho zote zinazozalishwa nchini zitabanguliwa na kuondokana na kuuza korosho ghafi nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo tarehe 18 Agosti, 2023 Jijini Tanga na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho mwaka 2023.
"Dhamira na shabaha ya Serikali yetu chini ya uongozi mahiri wa Mh. Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha zao la korosho linachangia kuongeza ajira na kipato kwa wakulima kupitia uongezaji wa thamani.
Na ndiyo maana jumla ya ekari 1,575.5 zimetengwa katika Halmashauri ya Nanyamba Mkoani Mtwara ambazo zitatumika kujenga Kongani ya viwanda vya kuchakata korosho na mazao yake kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2023/2024.
Vilevile, Zao la korosho pamoja na kuendelea kuwanufaisha wakulima, pia linaoongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni ambapo kwa msimu uliopita wa mwaka 2022/2023 limeingiza Dola za Kimarekani Milioni 226.9.
Kuendelea kuuza korosho ghafi nje ni kupeleka ajira zetu, utajiri wa wakulima wetu na mapato ya nchi yetu, hili hatuwezi kulikubali na lazima lifike mwisho ifikapo mwaka 2026/2027. Ni lazima tuhakikishe zaidi ya tani 300,000 zinabanguliwa nchini kwa mwaka ikiwa ni pamoja na kukamua maganda ya korosho hizo
Serikali inaendelea kuboresha kanzidata ya wakulima kwa kupima mashamba kwa kuchukua Coordinates, kuhesabu idadi ya mikorosho kwa kutumia mfumo wa satelites, kupiga picha mkulima, kuchukua alama vidole na kumpatia mkulima namba maalum ya utambulisho ambayo ataitumia kupata pembejeo na kuuza korosho zake.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Korosho, Brig. Gen. Aloyce Mwanjile aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mikakati ya kuinua tasnia ya korosho ambayo itawezesha kufikia lengo la kuzalisha tani 700,000 za korosho ghafi ifikapo mwaka 2025/2026.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Waziri Kindamba aliishukuru kwa niaba ya wananchi wa Tanga kwa kuchagua Mkoa wao kuwa mwenyeji wa Mkutano huo na kubainisha kuwa kutaongeza chachu na kuimarisha uzalishaji wa zao la korosho.