Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ameahidi kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana wanamichezo Jijini Dodoma kupitia mashindano ya MAVUNDE CUP ambayo yanafanyika kwa ngazi za kata.
Mavunde ameyasema hayo jana wakati akihitimisha mashindano ya UVCCM MAVUNDE CUP kata ya Makutupora ambayo fainali yake ilichezwa jana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Veyula kati ya Makutupora FC na Veyula FC,ambapo Timu ya Veyula FC ilitawazwa kuwa mabingwa wapya kwa ushindi wa 1-0.
“Nazipongeza timu zote zilizoshiriki katika mashindano haya kwa kuonesha nidhamu ya hali ya juu katika muda wote wa mashindano haya.
Nimefurahishwa na vipaji vikubwa vya wachezaji nilivyoviona hapa katika mchezo huu wa leo na hii ni hazina kubwa sio kwa Dodoma tu bali hata Taifa kwa ujumla.
Nitaendelea kuibua vipaji na kuviendeleza na hasa katika kuwatafutia fursa mbalimbali vijana wote wanaoshiriki mashindano haya.
Mwaka jana mashindano haya yametoa wachezaji wengi ambao wanashiriki katika mashindano ya Ligi ya U-20 ambayo ni daraja kuelekea mafanikio yao”Alisema Mavunde
Naye Diwani wa Kata ya Makutupora Mh. Eliya Lenjila amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuandaa mashindano hayo ambayo yameleta umoja na mshikamano miongoni mwa Vijana wa kata hiyo sambamba na burudani kubwa ambayo wananchi wa kata hiyo wameipata kwa muda wote wa mashindano.
Akisoma risala,Katibu wa UVCCM Kata ya Makutupora Cde. Angel Lyimo amesema moja ya mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia mashindano ni hamasa kubwa ya vijana wengi kushiriki katika michezo ambayo imewaepusha na makundi mbalimbali yenye kuathiri tabia njema za Vijana.