Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Tanzania inaunga mkono matumizi ya mfumo wa ununuzi wa pamoja wa dawa na vifaa tiba wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuharakisha uzalishaji wa dawa ya Lenacapavir barani Afrika.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Novemba 12, 2026, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, jijini Durban nchini Afrika Kusini, wakati wa kikao cha Mawaziri wa Afya na wenye dhamana ya masuala ya UKIMWI wa SADC, ambapo Tanzania imesisitiza umuhimu wa Mpango wa Ununuzi wa Pamoja wa Dawa na Vifaa Tiba wa SADC (SADC Pooled Procurement Services – SPPS) katika kukuza uzalishaji wa dawa ndani ya ukanda huo.
Amesema mpango huo utasaidia kuunganisha mahitaji ya dawa na vifaa tiba ya nchi wanachama, hatua itakayowezesha upatikanaji wa soko kubwa na la uhakika kwa wazalishaji wa dawa katika ukanda wa SADC, kuongeza uwekezaji katika viwanda vya ndani na kuimarisha ushindani wa bidhaa zinazozalishwa barani Afrika.
Aidha, amesema Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti ya SPPS ili kuhakikisha inaanza kazi kwa ufanisi, kwa kuzingatia mahitaji ya nchi wanachama na matokeo yanayotarajiwa, huku wananchi wakinufaika na upatikanaji endelevu wa dawa na vifaa tiba muhimu.
Dkt. Samizi ameongeza kuwa Tanzania ipo tayari kutoa dhamira ya kisiasa, msaada wa kitaasisi na rasilimali zinazohitajika ili kuhakikisha Sekretarieti ya SPPS inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo ya SADC katika ushirikiano wa afya, maendeleo ya viwanda na upatikanaji wa dawa muhimu.
Amesema kuunganisha mahitaji ya Lenacapavir dawa inayotumika katika kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa bora na salama kwa gharama nafuu.katika nchi za SADC kutatoa uhakika wa soko na kiwango cha uzalishaji kinachohitajika kwa wazalishaji, hivyo kuwezesha dawa hiyo kuzalishwa barani Afrika kwa ajili ya Waafrika na kuwafikia watu wanaohitaji huduma za kinga dhidi ya VVU.
Aidha, Tanzania imesaini Hati ya Makubaliano ya Kuanzisha SPPS (SPPS Charter), itakayoiweka taasisi hiyo kuwa chombo maalumu cha SADC, huku ikizishukuru nchi wanachama kwa ushirikiano wao uliofanikisha hatua hiyo na kutoa wito kwa nchi ambazo hazijasaini kufanya hivyo mapema ili kuruhusu taasisi hiyo kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi.
Vilevile, Tanzania imependekeza kuanzishwa kwa maadhimisho ya kila mwaka ya Siku ya SPPS (SPPS Day) wakati wa mikutano hiyo ya kikanda, pamoja na kuteuliwa kwa Kinara wa SPPS (SPPS Champion) atakayesaidia kutangaza na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa mpango huo katika nchi wanachama.
