WIZARA YA AFYA YATOA TAHADHARI KUHUSU EBOLA, YASEMA HAKUNA MGONJWA TANZANIA


Wizara ya Afya imetoa tahadhari kwa wiananchi kuhusu tishio la ugonjwa wa Ebola kufuatia mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuripotiwa kwa mgonjwa wa ugonjwa huo nchini Kenya aliyesafiri kutoka DRC.

Hata hivyo, Wizara hiyo imesisitiza kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola aliyeripotiwa nchini Tanzania, huku Serikali ikiendelea kuimarisha hatua za kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini.

Katika taarifa iliyotolewa jijini Dodoma leo, Oktoba 21, 2026, Wizara ya Afya imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha uchunguzi wa afya kwa wasafiri katika viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu, pamoja na kufuatilia taarifa za wagonjwa katika jamii na vituo vya kutolea huduma za afya.

Hatua nyingine zinazotekelezwa ni kuimarisha utayari wa vituo vya afya, upatikanaji wa dawa na vifaa vya kujikinga na tiba, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili kukabiliana na ugonjwa huo endapo utaingia nchini.

Aidha, Serikali imehuisha na kusambaza Mwongozo wa Wasafiri Na. 18 wa Oktoba 17, 2026, unaoelekeza hatua za kiafya zinazopaswa kuzingatiwa na wasafiri wote wanaoingia nchini.

Wizara hiyo imeeleza kuwa Ebola huambukizwa kwa kugusa majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo, yakiwemo damu, mkojo, mate, matapishi na jasho, pamoja na kugusa vitu vilivyotumiwa na mtu mwenye maambukizi.

Ugonjwa huo pia unaweza kuambukizwa kwa kugusa wanyama pori wenye maambukizi, wakiwemo popo na jamii ya sokwe, au mizoga yao.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa, uchovu wa mwili, maumivu ya misuli na kichwa, kutapika na kuharisha. Katika baadhi ya wagonjwa, ugonjwa huo unaweza kusababisha kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili, zikiwemo puani, machoni, masikioni na katika njia za haja kubwa au ndogo.

Kutokana na tishio hilo, Wizara ya Afya imewataka wananchi kuzingatia usafi wa mikono kwa kunawa mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka kugusa majimaji ya mwili wa watu wenye dalili zinazofanana na Ebola, pamoja na kutogusa vitu walivyovitumia.

Pia, wananchi wametakiwa kuwahi katika kituo cha afya kilicho karibu wanapopata dalili zinazofanana na za ugonjwa huo na kutoa taarifa kwa kupiga simu bila malipo kupitia namba 199 wanapomuona mtu mwenye dalili hizo.

Wizara  imesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wataalamu wa afya katika usimamizi wa mazishi ya watu wanaofariki wakiwa na dalili zinazofanana na Ebola, kuepuka kugusa wanyama pori wanaoweza kuwa na maambukizi na mizoga yao, pamoja na kufuatilia taarifa kutoka vyanzo rasmi vya Serikali ili kuepuka upotoshaji.

Kwa upande wa watoa huduma za afya, Wizara imewataka kuimarisha utayari wa kutambua mapema dalili zinazoweza kuashiria Ebola, kutoa taarifa kwa wakati na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa.

Aidha, imewataka kuzingatia kikamilifu kanuni za kuzuia na kudhibiti maambukizi, ikiwemo usafi wa mikono na matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga kulingana na tathmini ya hatari, ili kulinda afya zao, wagonjwa na jamii kwa ujumla.

Wizara ya Afya imewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na wataalamu wa afya na kuzingatia maelekezo yanayotolewa, huku Serikali ikiendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa huo nje ya mipaka ya nchi na kuchukua hatua zinazohitajika kuimarisha usalama wa afya ya umma nchini Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post