Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imewezesha ujenzi wa minara saba na uboreshaji au uanzishwaji wa studio tano za Redio Jamii kwa gharama ya Shilingi bilioni 5.696, hatua inayolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa kwa wananchi katika jamii mbalimbali.
Waziri Kairuki ameyasema hayo Oktoba 20, 2026, wakati akiwasilisha taarifa kuhusu uimarishaji wa mawasiliano kupitia Redio Jamii mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bungeni jijini Dodoma.
Aidha, ameeleza kuwa UCSAF imeandaa mwongozo wa utoaji wa ruzuku kwa vituo vya Redio na Televisheni Jamii ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usawa katika ugawaji wa rasilimali, sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb.), ameishauri Serikali kuongeza kasi ya kuwezesha uanzishwaji wa vituo vya Redio Jamii katika mikoa ambayo bado haijafikiwa, ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo.
Hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kupanua upatikanaji wa taarifa, kuimarisha mawasiliano ya kijamii na kuongeza fursa kwa wananchi kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
