SERIKALI YAAHIDI KUENDELEZA BIASHARA NCHINI WAKATI WA KUFUNGA MAONESHO YA NNE YA TANZANITE MANYARA TRADE FAIR


Serikali imehitimisha kwa mafanikio Maonesho ya Nne ya Biashara ya Tanzanite Manyara Trade Fair (TMTF 2026) yaliyofungwa rasmi tarehe 21 Oktoba 2026 katika Viwanja vya Tanzanite Kwaraa, Babati – Manyara. Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bw. Ephraim Balozi Mafuru, alihudhuria kama mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (MB). Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya uwekezaji na biashara, wakiwemo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, viongozi wa serikali, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo.  


Katika hotuba yake, Bw. Mafuru aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi. Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora na kutumia vifungashio vyenye chapa ya Made in Tanzania ili kukuza soko la bidhaa za Tanzania na kulinda utambulisho wa Taifa. Aidha, aliongeza kuwa ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni lazima wazalishaji wa mchele na vitunguu wa Manyara waache kusafirisha mazao ghafi kwa mfumo wa “lumbesa” kwenda nchi jirani. Badala yake, waongeze thamani ya mazao nchini kwa kutumia vifungashio vya kilo mbili, tano hadi ishirini, vyenye nembo ya Made in Tanzania, na kisha kuuza bidhaa hizo nje ya nchi ili kuongeza ajira na mapato ya kigeni kupitia mauzo ya nje.  


Kwa upande wake, Meneja wa Chemba ya Taifa ya Biashara Mkoa wa Manyara, Lerunde Laizer, alisema lengo kuu la maonesho hayo ni kuwakutanisha wafanyabiashara na masoko, pamoja na kuhakikisha wajasiriamali wanapata maarifa, fursa na taarifa sahihi za kibiashara. Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara Mkoa wa Manyara, Mussa Msuya, alieleza kuwa maonesho hayo yamewapa wafanyabiashara fursa kubwa ya kuonesha na kutangaza bidhaa zao kwa wadau mbalimbali, na kusisitiza kuwa mkoa wa Manyara unakua kiuchumi hivyo wawekezaji wanapaswa kutumia fursa hiyo kuwekeza ndani ya mkoa.  


Takwimu za maonesho zilionesha mafanikio makubwa: washiriki walifikia 180 mwaka 2026 ikilinganishwa na 117 mwaka 2024, watembeleaji walikuwa 14,530 wakiwemo wageni 30 kutoka nje ya nchi, na mabanda ya maonesho yalifikia 74. Aidha, takwimu za uzalishaji wa bidhaa kuu za Manyara zilionesha mchango mkubwa wa kiuchumi: mahindi tani 440,842 (TZS 198–265 bilioni), alizeti tani 113,400 (TZS 136 bilioni), vitunguu tani 85,000 (TZS 102–153 bilioni), Tanzanite kilo 500–640 (TZS 48 bilioni), na mtama tani 7,500 (TZS 2.6 bilioni).  


Katika hitimisho, Bw. Mafuru alitoa shukrani kwa Serikali ya Mkoa wa Manyara, wadhamini, washirika, taasisi, wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wote walioshiriki. Alisisitiza kuwa kufungwa kwa maonesho haya si mwisho wa shughuli za kibiashara, bali ni mwanzo wa kutekeleza fursa na mawazo yaliyopatikana. Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, alitangaza rasmi kufungwa kwa Maonesho ya Nne ya Tanzanite Manyara Trade Fair (TMTF 2026) tarehe 21 Oktoba 2026, na kuwatakia washiriki mafanikio katika utekelezaji wa mikataba na uwekezaji waliopata.

Post a Comment

Previous Post Next Post