MBUNGE wa Jimbo la Kondoa Mjini, Mhe. Mariam Ditopile, ameungana na ujumbe mzito wa Baraza la Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri hiyo katika ziara ya kimkakati Jijini Tanga, yenye lengo la kujifunza utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ya maendeleo ili kuboresha huduma kwa wananchi wa Kondoa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ditopile aliweka wazi dhamira ya ujumbe huo akisisitiza kuwa wao kama viongozi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha fedha zinazoletwa na Serikali zinaleta tija na kubadilisha maisha ya wananchi.
"Sisi ni wapanga maendeleo, watekelezaji, na wasimamizi wa miradi ya maendeleo, hususani kusimamia fedha nyingi zinazoletwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye halmashauri yetu. Kuja kwetu Tanga kutatuwezesha kuongeza ujuzi na kasi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025-2050, ambayo zaidi ya asilimia 70 itatekelezwa na sekta binafsi," alisema Ditopile.
Ujumbe huo ulitembelea miradi mbalimbali Jijini Tanga ikiwemo Dampo la Kisasa la kukusanya taka ngumu lililopo Mtaa wa Mpirani, Kata ya Chongoleani, pamoja na mradi mkubwa wa Maegesho ya Malori uliopo Kange, ujenzi wa shule za ghorofa na Bandari ya Tanga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Almas Nyangasa (ambaye aliwahi kuwa mtangazaji maarufu wa ITV), alisema ameambatana na wataalamu ili kujifunza matumizi sahihi ya ardhi ndogo kujenga majengo yanayoleta faida kwa wananchi.
"Huu mradi wa kukusanya taka, tukienda kuutekeleza baada ya kujifunza hapa utaleta tija, utaongeza mapato ya halmashauri, lakini pia utatoa ajira kwa watu wetu," alisema DC Nyangasa. Pia, alimpongeza Rais kwa uboreshaji wa Bandari ya Tanga na kufungua barabara ya Handeni - Kondoa hadi Singida, hatua itakayochochea uchumi wa wilaya yao.
