WIZARA YA NISHATI YAPONGEZWA KUTEKELEZA MAAGIZO YA KAMATI


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutekeleza maagizo ya Kamati hiyo ya kuwataka Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini kushirikiana katika kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati katika sekta ya madini.

Mhe. Mgalu ameyasema hayo Septemba 3, 2026, jijini Dodoma, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Mponvu–GGM ya msongo wa kilovolti 220 (kV) pamoja na Kituo cha Kupoza Umeme kitakachojengwa katika eneo la GGM, Geita.

Amesema anafurahishwa na hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo, hususan kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa migodi ya wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.

“Tunafarijika kuona maelekezo tuliyoyatoa katika kikao cha Kamati yakitekelezwa. Ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini umewezesha kufikiwa kwa hatua hii kubwa ya kupeleka umeme wa uhakika katika maeneo ya migodi kupitia mradi wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 63,” amesema Mhe. Mgalu.

Aidha, amekumbusha ziara ya Kamati hiyo iliyofanyika Machi 15, 2026, katika Kituo cha Mponvu, Geita, ambapo pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, walijionea uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 50 uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika miundombinu ya umeme.

Amesema ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 220 utakaoiwezesha migodi ya GGM kupata umeme wa uhakika ni hatua muhimu katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa ufanisi na tija zaidi.

“Upatikanaji wa umeme wa uhakika utasaidia migodi kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza uzalishaji na hatimaye kuchangia katika kukuza pato la Taifa kupitia sekta ya madini,” amesema.

Mhe. Mgalu pia ameipongeza TANESCO pamoja na Bodi ya Wakurugenzi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuboresha huduma ya umeme nchini, akihusisha jitihada hizo na kauli mbiu ya Shirika isemayo “Tunaangaza Maisha Yako.”

Amesema jitihada za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi wa kisasa na kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Post a Comment

Previous Post Next Post