Tanzania imepewa nafasi ya Uenyekiti Mwenza katika Jukwaa la Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi linalofanyika jijini Beijing, China, huku Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akishiriki katika nafasi hiyo.
Nafasi hiyo imetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, ambayo ni mwenyeji wa jukwaa hilo, ambapo Prof. Mbarawa anashirikiana na Waziri wa Uchukuzi wa China, Mhe. Liu Wei. Jukwaa hilo limewakutanisha zaidi ya mawaziri 20 wa sekta ya uchukuzi kutoka nchi mbalimbali duniani.
Jukwaa hilo la siku tatu linajadili masuala ya maendeleo endelevu ya sekta ya uchukuzi, kubadilishana maarifa na uzoefu, pamoja na kuhamasisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa China (Global Development Initiative - GDI).
Akizungumza katika jukwaa hilo, Prof. Mbarawa amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya uchukuzi, ikiwemo ujenzi wa reli za kisasa, barabara, bandari na viwanja vya ndege.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuboresha usafirishaji, kuunganisha maeneo ya vijijini na mijini, kuimarisha biashara na kuchochea ustawi wa wananchi.
Prof. Mbarawa pia ametumia fursa hiyo kuwaalika taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya uchukuzi nchini.
“Tanzania ina fursa nyingi kupitia Sekta ya Uchukuzi, hivyo ninawaalika taasisi za serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza kwenye sekta ya Uchukuzi Tanzania,” amesema Prof. Mbarawa.
Ushiriki wa Tanzania katika nafasi hiyo unatoa fursa ya kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya uchukuzi na miundombinu, ikiwemo kubadilishana uzoefu, teknolojia na kutafuta fursa za uwekezaji.
Tanzania na China zina ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya uchukuzi, ukiwemo mradi wa reli ya TAZARA pamoja na usafiri wa majini kupitia SINOTASHIP.
