SALOME ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MRADI WA BILIONI 63 KUSAMBAZA UMEME MAENEO YA MIGODI


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 63 kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 (kV) kutoka Mpomvu hadi Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), pamoja na ujenzi wa kituo kipya cha kupokea na kupoza umeme cha 220kV chenye transfoma yenye uwezo wa MVA 90.

Hafla ya utiaji saini mkataba huo imefanyika Septemba 3, 2026, katika Hoteli ya Vizano jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Salome amesema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa kampuni za Sihotech Engineering Company na Sieyuan Electric Company Limited, kwa lengo la kuongeza uwezo wa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya migodi na kuchochea shughuli za uzalishaji.

Amesema mradi huo ni sehemu ya Mradi wa Mapato wa TANESCO, unaojumuisha  awamu ya kwanza yenye jumla ya miradi 52 ya usambazaji umeme kwa wateja wakubwa na miradi mitatu (3) ya usafirishaji umeme inayohusisha maeneo ya migodi.

Aidha, Mhe. Salome amekumbusha hatua iliyofikiwa tarehe 13 Agosti 2024, ambapo kituo cha kupokea na kupoza umeme chenye uwezo wa MW 34 kilizinduliwa na kuwezesha Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Hatua hiyo ilisaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa mgodi pamoja na kulinda mazingira kwa kupunguza matumizi ya mafuta katika uzalishaji wa umeme.

“Awali GGM ilikuwa ikitumia takribani Shilingi bilioni 10 hadi 13.4 kwa mwezi kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta. Baada ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, imeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama hizo. Kadhalika, kwa kutumia umeme wa gridi, sote tumeokoa mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa,” amesema Mhe. Salome.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi mpya wa msongo wa kilovoti 220 utaongeza uwezo wa kusafirisha na kusambaza umeme kwa Mgodi wa GGM, kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme, kuongeza mapato ya TANESCO na kuchochea ajira, uwekezaji na ukuaji wa uchumi.

Mhe. Salome amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha miundombinu ya nishati ili iwe kichocheo cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayotambua nishati kuwa miongoni mwa vichocheo muhimu vya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Ndg. Lazaro Twange, amesema Shirika limeanza kuihudumia GGM tangu mwaka 2024 kwa kuipatia umeme wa MW 16. Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa mitambo na shughuli za uchimbaji, mahitaji ya umeme yameongezeka na kufanya miundombinu iliyopo kutotosheleza mahitaji hayo.

Amesema utekelezaji wa mradi huo utasaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme na kuhakikisha GGM inaendelea kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya shughuli zake za uzalishaji.

Naye, Mwakilishi wa wamiliki wa Mgodi wa GGM, ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuiomba kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kasi na kukamilika kwa wakati, ili mgodi huo uweze kuendelea na shughuli za uchimbaji na uzalishaji, hatua itakayochangia zaidi katika kukuza pato la Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post