NAIBU WAZIRI SAMIZI AKAGUA MAANDALIZI YA UZINDUZI WA RAMANI YA AFYA YA MAMA NA MTOTO AFRIKA


Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, amekagua maandalizi ya mkutano wa uzinduzi wa Ramani ya Umoja wa Afrika ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Balehe (RMNCAH) 2026–2030, unaotarajiwa kufanyika Septemba 9, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Akikagua maandalizi hayo, Mhe. Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili hadhi ya mkutano huo muhimu unaotarajiwa kuwakutanisha viongozi na wadau mbalimbali wa afya kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.

Amesema mkutano huo una umuhimu mkubwa katika kuendeleza juhudi za Bara la Afrika za kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto na balehe kupitia utekelezaji wa agenda ya “Advancing the Three Zeros for a Healthier Africa.”

Uzinduzi wa Ramani hiyo unatarajiwa kufanywa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Bingwa wa Umoja wa Afrika (AU) katika masuala ya Afya ya Mama na Mtoto.

Mhe. Dkt. Samizi amesema Tanzania inajivunia kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa tukio hilo muhimu na kwamba maandalizi yanapaswa kuakisi uwezo na hadhi ya nchi katika kuandaa na kusimamia mikutano ya kimataifa.

Ameitaka timu inayosimamia maandalizi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kila eneo la maandalizi, ikiwemo mapokezi ya wageni, ukumbi wa mkutano na huduma nyingine muhimu, linakamilika kwa wakati.

Ramani ya RMNCAH 2026–2030 inalenga kuunganisha viongozi wa Afrika na wadau mbalimbali katika kuharakisha hatua, uwekezaji na uwajibikaji kwa lengo la kuboresha afya ya mama, watoto, vijana na balehe barani Afrika.

Post a Comment

Previous Post Next Post