Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE umekamilisha maandalizi ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 58 kwa kiwango cha lami katika halmashauri ya wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.
Hatua hiyo imekuja sambamba na kuanza kwa zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaostahili ambao maeneo yao yanaathiriwa na utekelezaji wa mradi huo hatua inayofungua njia kwa kuanza kwa ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.
Akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa zoezi la ulipaji fidia, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Mhe. Grace Kingalame amewataka watendaji kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi, usawa na haki ili kila mwananchi anayestahili alipwe kwa mujibu wa taratibu.
"Ninaimani kuwa wataalamu wetu mmejipanga vizuri na sitarajii kupata malalamiko katika zoezi hili", amesema.
Kwa upande wake, Mhandisi wa miradi kutoka TARURA, Ephraim Kalunde amesema Wakala umezingatia hatua zote muhimu za maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo ikiwemo mchakato wa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi.
"Wakala umejipanga na hadi tunafikia hatua hii kila hatua imezingatiwa hivyo ni imani yetu kuwa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha mradi litafanyika kwa ufasaha", amesema Mhandisi Kalunde.
Naye, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbogwe Mhandisi Patrick Chacha amesema hadi sasa mikataba miwili ya utekelezaji wa miradi hiyo imeshapata makandarasi na kusainiwa hatua inayoweka mazingira ya kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo.
Akielezea juu ya mchakato wa ulipaji wa fidia kwa wananchi, Meneja wa Benki ya CRDB Wilaya ya Mbogwe Bw. Lwaga Mwakalinga amesema kuwa Benki hiyo imejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya uhifadhi wa fedha na kuhakikisha fedha hizo zinawanufaisha.
"Tumetoa elimu ya kutosha kwa wananchi na tunaanza zoezi la kuwafungulia akaunti kwa wale wasiokuwa nazo pia tumewaelekeza kufika ofisini kwa watakaohitaji elimu ya uwekezaji", amesema.
Akielezea juu ya hatua iliyofikiwa katika zoezi hilo, mmoja wa wanufaika wa mradi huo Bw. George Bilabika amesema kuwa barabara hizo zitasaidia katika kukuza uchumi wa wilaya hiyo kwani kuna mazao mengi ya biashara.
