WAZIRI WA ULINZI NA JKT AFANYA ZIARA YA KIKAZI SHIRIKA LA NYUMBU, KUJIONEA UTENDAJI WAKE


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Shirika la Tanzania Automotive Technology Centre (TATC), maarufu kama NYUMBU, lililopo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kujionea utendaji na utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo. 

Katika ziara hiyo, Waziri Nyansaho alitembelea maeneo mbalimbali ya Shirika la NYUMBU, ambalo ni la kimkakati na linamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ili kujionea shughuli zinazotekelezwa na namna shirika hilo linavyotekeleza majukumu yake katika kuunga mkono shughuli za ulinzi, maendeleo ya teknolojia na uchumi wa Taifa. 

Akizungumza na uongozi na menejimenti ya shirika hilo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Luteni Jenerali na Balozi mstaafu Paul Meela, Waziri Nyansaho amesema ziara hiyo imelenga kujionea kwa karibu utendaji wa Shirika la NYUMBU, pamoja na utekelezaji wa majukumu yake ya kimkakati na kiulinzi, hususan katika kuchangia maendeleo ya uchumi na ustawi wa Taifa.

Aidha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameupongeza uongozi wa Shirika la NYUMBU kwa kazi zinazofanyika na kueleza matarajio ya Serikali ya kuona shirika hilo likizidi kutumia fursa zilizopo ili kuongeza mchango wake katika uchumi na ustawi wa Taifa. 

Amesisitiza kuwa shughuli zinazotekelezwa na Shirika la NYUMBU zinapaswa kwenda sambamba na matarajio ya Serikali ya kuhakikisha taasisi za umma zinatoa mchango madhubuti katika maendeleo ya Taifa na utoaji wa huduma zenye manufaa kwa jamii. 

Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Othman, wajumbe wa Bodi ya Shirika la NYUMBU, pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania. 

Tanzania Automotive Technology Centre (TATC), maarufu kama NYUMBU, ni shirika la umma chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa linalojihusisha na utengenezaji, ukarabati na ubunifu wa teknolojia katika eneo la vyombo vya moto, vipuri na vifaa vya uhandisi.

Post a Comment

Previous Post Next Post