WANANCHI, WADAU WAMWAGIA SIFA REA MAONESHO YA NANE NANE DODOMA


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulikuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane 2026 yaliyofungwa hivi karibuni jijini Dodoma, huku wananchi na wadau mbalimbali wakipongeza ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika utoaji wa huduma.

Katika maonesho hayo yaliyohitimishwa rasmi Agosti 8, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye viwanja vya Nzuguni, REA ilikuwa miongoni mwa taasisi zaidi ya 400 za Serikali na sekta binafsi zilizoshiriki.

Uchunguzi uliofanywa katika banda la REA umebaini kuwepo kwa mtiririko mkubwa wa wageni waliofurika kujionea matumizi ya teknolojia ya kisasa ya runinga za kidijitali (Smart Touch Screen TV) pamoja na mabango yenye lugha rahisi ya picha yanayoelezea miradi ya kusambaza nishati mbalimbali vijijini.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Bi. Suzan Ngwegwe, mkazi wa Kitongoji cha Wala B kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, alieleza kufurahishwa kwake na kasi ya upatikanaji wa taarifa za maendeleo ya umeme wa vijijini.

“Nimefurahi kuona taarifa za kitongoji changu zipo kwenye runinga ya maonesho na ndani ya muda mfupi nimepata majibu. Hapo kabla sikuwa nikifahamu, na nimeenda mabanda mengine sikuona huduma kama hii. Nawapongeza sana REA,” alisema Bi. Suzan.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mstaafu, Bi. Asia Abdallah, alisifu ubunifu wa wakala huo katika kupanga mabango yanayotumia lugha rahisi na picha zinazojieleza, akibainisha kuwa mfumo huo unamsaidia hata mtu asiyejua kusoma kuelewa kwa haraka.

“Hongera kwa ubunifu wa kutumia Smart Touch TV Screen. Taarifa zinaonekana ndani ya muda mfupi; unaona idadi ya vijiji na vitongoji vyenye umeme, na vile vilivyo kwenye matazamio ya kufikiwa,” alisema Bi. Asia.

Kwa upande wa usimamizi na uwajibikaji, Mkuu wa wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, alisema maonyesho hayo ni kielelezo cha kazi kubwa inayofanywa na REA nchini kote.

Wakati huo huo, wadau wa mazingira wamepongeza mkakati wa REA wa kuwapa nafasi wajasiriamali wa sekta binafsi kutangaza teknolojia za nishati safi ya kupikia.

Bw. Ally Salehe, mdau wa mazingira kutoka mkoani Manyara, alisema miradi ya nishati safi inayochochewa na REA inalenga kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, hatua itakayookoa misitu ya vijijini na kulinda afya za kina mama dhidi ya magonjwa ya mfumo wa hewa.

Post a Comment

Previous Post Next Post