RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Kizimkazi na maeneo jirani kutunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni msingi wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Akizungumza leo Alhamisi, Agosti 13, 2026 visiwani Zanzibar, mara baada ya kuzindua Mradi wa Maji Kizimkazi, Rais Samia amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali unapaswa kulindwa ili uweze kuwasaidia wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
“Ni wajibu na ni lazima tutunze miradi hii kama tunavyotunza macho yetu. Miradi hii ni fursa zetu, ni uchumi na ustawi wa maisha yetu,” amesema Rais Samia.
Amesema miradi hiyo imeletwa kutokana na kuwepo kwa amani nchini, hivyo amewataka wananchi kuendelea kuitunza amani yao ili Tanzania iweze kupata maendeleo zaidi.
“Miradi hii tumeweka kuileta kwa sababu nchi yetu ina amani. Niombe sana ndugu zangu tuendelee kutunza amani yetu ili tupate maendeleo zaidi,” amesema.
Rais Samia amesema kaulimbiu ya “Mapinduzi Daima” inapaswa kuakisi mapinduzi ya maendeleo, akieleza kuwa Mapinduzi yalishafanyika, huku Mapinduzi ya sasa yakilenga kubadili hali iliyopo na kuleta maendeleo bora zaidi.
“Tunaposema Mapinduzi Daima, Mapinduzi ya sasa ni maendeleo,” amesema, huku akiwataka wananchi kuyatunza Mapinduzi yao.
Aidha, amesema uwezo wa Mradi wa Maji Kizimkazi umezingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye, ambapo uwezo wake ni mara mbili ya mahitaji ya sasa kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa miji.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wananchi kuipenda na kuilinda miundombinu hiyo kwa kuwa fedha nyingi zimetumika kuitekeleza, hivyo inapaswa kutunzwa ili iweze kunufaisha wananchi leo na kesho..
Tags
Afya
