TRC NA FS ENGINEERING ITALIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA UTAALAMU NA UENDESHAJI WA MIUNDOMBINU YA RELI


Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kampuni ya FS Engineering S.p.A ya Italia zimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuimarisha uwezo wa kiufundi, uhandisi na usimamizi wa miundombinu ya reli nchini Tanzania.

Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Roma, Italia leo Jumatano Agosti 5, 2026, katika Makao Makuu ya Wizara ya Miundombinu na Uchukuzi nchini humo, yakilenga kuweka mfumo wa ushirikiano katika maendeleo ya miundombinu ya reli, huduma za uhandisi, ujenzi wa uwezo wa kitaasisi na matumizi ya teknolojia za kisasa kati ya TRC na FS Engineering S.p.A.

Hati hiyo imesainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu na Meneja Mkuu wa FS Engineering, Prof. Dario Lo Bosco, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Masanja Shiwa pamoja na Mkurugenzi Msimamizi wa ITS Engineering, Mhandisi Michele Titton katika hafla iliyohudhuriwa na Naibu Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia, Mheshimiwa Edoardo Rixi, na Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mbarawa amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa TRC kuendeleza na kusimamia miradi ya reli kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Amesema Tanzania inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya usafiri wa reli kupitia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ukarabati wa mtandao wa reli ya zamani na uboreshaji wa huduma za usafiri wa reli ili kuchochea ukuaji wa uchumi, biashara ya kikanda na ushindani wa kiuchumi.

Ameongeza kuwa kupitia makubaliano hayo, TRC na FS Engineering zitashirikiana katika uchambuzi wa fursa za maendeleo ya miundombinu ya reli, uandaaji wa miongozo ya usimamizi wa miundombinu, mafunzo kwa wataalamu wa TRC, pamoja na kusaidia uanzishwaji wa uwezo wa uhandisi ndani ya Shirika hilo.

Kwa upande wake, Prof. Dario Lo Bosco,  amesema FS Engineering imejipanga kutumia uzoefu wake katika usanifu wa kidijitali, uhandisi wa kisasa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu kusaidia maendeleo ya mifumo ya usafiri yenye ufanisi, endelevu na inayotumia teknolojia za kisasa.

Amesema ushirikiano kati ya FS Engineering, TRC na ITS Engineering utasaidia ubadilishanaji wa utaalamu na kuimarisha uhusiano kati ya Italia na Tanzania katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya miundombinu ya usafiri ya baadaye.

Aidha, FS Engineering itawezesha upatikanaji wa utaalamu wa mifumo ya kidijitali ikiwemo Digital Control Room, jukwaa la kisasa linalowezesha ufuatiliaji na usimamizi wa miradi mikubwa ya miundombinu kwa kutumia teknolojia za kidijitali, drones na uchanganuzi wa takwimu.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa TRC katika usimamizi wa miradi ya reli na kusaidia Tanzania kujenga mfumo wa usafiri wa reli wa kisasa, salama na endelevu.

Post a Comment

Previous Post Next Post