TIBA ASILI ZENYE USHAHIDI WA KISAYANSI ZIJUMUISHWE KATIKA MFUMO RASMI WA AFYA


Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema ipo haja ya kuongeza kasi ya utafiti, ubunifu na uwekezaji katika tiba asili ili tiba zenye ushahidi wa kisayansi ziweze kujumuishwa katika mfumo rasmi wa utoaji huduma za afya nchini.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 28, 2026 Jijini Mbeya na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)  Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya kwa niaba ya Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tano la Kisayansi la Tiba Asili liliandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Amesema tiba asili ni sehemu ya maisha na utamaduni wa Watanzania na inaendelea kuwa na mchango katika afya ya jamii, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza tafiti za kisayansi na uwekezaji katika uzalishaji wa dawa za tiba asili ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya usalama, ubora na ufanisi.

Aidha, amesema ujumuishaji wa tiba asili katika mfumo rasmi wa afya unahitaji ushirikiano wa watafiti, wataalamu wa tiba asili na tiba za kisasa, taasisi za utafiti, vyuo vikuu, waangalizi na watunga sera.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuiwezesha NIMR katika utafiti, ufuatiliaji na uhakiki wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa za tiba asili, sambamba na kuimarisha uwezo wa maabara na mifumo ya uzalishaji.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni kuendelea kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ya kuhakikisha dawa za tiba asili zenye ushahidi na ubora unaokubalika zinapatikana katika hospitali na vituo vya afya ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Aidha, ametoa wito kwa wadau kuongeza kasi ya tafiti na ugunduzi wa tiba asili, huku akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kulinda maarifa ya tiba asili kama sehemu ya urithi wa kitamaduni na rasilimali ya taifa.

Ametoa wito kwa washiriki wa kongamano hilo kuyafanyia kazi matokeo ya majadiliano na kuimarisha ushirikiano ili tiba asili zenye ushahidi wa kisayansi ziendelee kuchangia katika usawa wa afya, ubunifu na maendeleo endelevu nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post