TAMISEMI KUTANGAZA MKUTANO WA PILI WA KIMATAIFA WA HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI ARUSHA


Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, inatarajia kuandaa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi utakaofanyika Septemba 9 hadi 11, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Mkutano huo utawakutanisha wataalamu wa afya, watafiti, watunga sera, vyuo vikuu, wabunifu wa teknolojia za afya pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amesema mkutano huo unafuatia mafanikio ya mkutano wa kwanza wa kimataifa uliofanyika Dodoma.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kuimarisha Mifumo ya Afya ya Msingi kuelekea Huduma za Afya kwa Wote”, huku ajenda kuu zikiwa ni kuboresha ufadhili wa huduma za afya, kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali watu na fedha, pamoja na kuimarisha ubora wa huduma.

Dkt. Mfaume amesema mkutano huo utatoa fursa kwa Tanzania kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya, ikiwemo hatua za kupunguza vifo vya wajawazito vinavyotokana na matatizo ya uzazi pamoja na vifo vya watoto chini ya miaka mitano.

Amesema zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hupata huduma kupitia mfumo wa afya ya msingi unaojumuisha huduma za ngazi ya jamii, zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya.

Kwa mujibu wa Dkt. Mfaume, mafanikio hayo yamechangiwa na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu, vifaa tiba na rasilimali watu. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, amesema hospitali za wilaya zaidi ya 129 zimejengwa, pamoja na vituo vya afya na zahanati zaidi ya 1,300.

Aidha, amesema mkutano huo utajadili matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za afya, tafiti, maboresho ya sera na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ya msingi.

Kwa upande wake, Dkt. Pius Kamana kutoka TAMISEMI amesema takribani asilimia 73 ya vituo vyote vya afya nchini ni vituo vya ngazi ya msingi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mfumo huo.

Dkt. Kamana amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za afya ya msingi, hivyo uwepo wa jukwaa hilo utasaidia kuongeza ufanisi, kubadilishana uzoefu na kupata maazimio yatakayoboresha zaidi huduma kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa changamoto za kiafya hazina mipaka, hivyo ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kujenga mifumo imara ya afya na kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazolikabili Bara la Afrika na dunia kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post