SERIKALI YATOA MIEZI SITA KUSAJILI MIUNDOMBINU MUHIMU YA TEHAMA


SERIKALI imebainisha na kutangaza Miundombinu Muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CII) katika sekta mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa mifumo muhimu dhidi ya changamoto na vitisho vya kiusalama.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatano Agosti 19, 2026 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya mwaka 2015, hususan Kifungu cha 28(1), kinachompa Waziri mwenye dhamana ya mawasiliano mamlaka ya kutangaza Miundombinu Muhimu ya TEHAMA.

Amesema CII inajumuisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta au mitandao, inayoshikika au isiyoshikika, ambayo ikishindwa kufanya kazi inaweza kusababisha madhara au athari za kiusalama, kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, sekta zinazohusika na miundombinu hiyo ni pamoja na habari na mawasiliano, fedha na benki, maji, afya, nishati, madini, usafirishaji, chakula na kilimo, ujenzi, uchumi wa buluu, mazingira na viwanda.

Sekta nyingine ni ulinzi, anga, elimu, utawala wa kiserikali, ulinzi wa raia, ardhi pamoja na usalama na utulivu wa umma.

Amesema Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kushirikiana na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi, imebainisha CII na kuandaa miongozo mitano inayohusu utambuzi na usimamizi wa CII, ukaguzi, tathmini ya hatari, uhakika na uhalisia wa data pamoja na mipango ya urejesho wa huduma baada ya janga.

Waziri Kairuki ametoa rai kwa wamiliki wa miundombinu hiyo kuhakikisha wanazingatia taratibu zilizowekwa ili miundombinu muhimu ya TEHAMA iweze kulindwa na kuendelea kutoa huduma muhimu kwa usalama.

Tangazo la Serikali Na. 147 la Juni 19, 2026 ndilo lililotangaza rasmi CII kwa ajili ya usajili na kupata ulinzi wa kisheria.

Muda wa usajili ni miezi sita kuanzia Juni 19 hadi Desemba 19, 2026, huku wamiliki wakitakiwa kutumia CII Portal kwa ajili ya usajili.

Post a Comment

Previous Post Next Post