NAIBU WAZIRI MWANA FA AKAGUA UWANJA WA CCM KIRUMBA, AAHIDI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO YA TAA


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mwana FA), ametembelea na kukagua hali ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha miundombinu ya michezo nchini.

Mhe. Mwinjuma ameambatana na Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, ikiongozwa na Katibu wa CCM Mkoa, Abdul Mtua, ambapo wamepata fursa ya kuona hali halisi ya uwanja huo pamoja na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuongeza matumizi na thamani ya uwanja huo kwa wananchi na wadau wa michezo.

Moja ya changamoto kubwa iliyobainika ni ukosefu wa mfumo wa taa unaowezesha uwanja kutumika kwa ufanisi nyakati za usiku. Hali hiyo imekuwa ikipunguza fursa za kufanyika kwa baadhi ya shughuli za michezo, hususan mechi na matukio yanayohitaji matumizi ya uwanja wakati wa usiku.

Akizungumza baada ya kupokea maombi hayo, Mhe. Mwinjuma ameahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na wadau pamoja na wapenda maendeleo ya michezo nchini, ili kuona namna changamoto ya taa inavyoweza kupatiwa ufumbuzi.

Hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, wa kuendelea kuwekeza na kuboresha miundombinu ya michezo ili iwe katika hali bora, salama na iweze kutumika ipasavyo na wananchi pamoja na Wanamichezo.

Post a Comment

Previous Post Next Post