Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema michezo ina umuhimu mkubwa katika malezi na makuzi ya watoto, kwa kuwa huwajengea ubunifu, tabia njema, nidhamu, heshima na ushirikiano.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 12, 2026, mara baada ya kuzindua Kiwanja cha Kufurahisha Watoto cha Kizimkazi, visiwani Zanzibar, akieleza kuwa michezo ni kichocheo muhimu katika kujenga utu, maadili na uwezo wa watoto kuchangamana na wengine pamoja na kukua kiakili.
Amesema viwanja hivyo havipaswi kutazamwa kama sehemu za burudani pekee, bali kama maeneo muhimu ambayo yamewekewa uwekezaji kwa ajili ya kuhakikisha watoto wanapata malezi na makuzi bora.
“Hatupaswi kuvitazama viwanja hivi kama sehemu ya burudani pekee bali tuvione kama sehemu ya msingi tuliyowekeza kwa ajili ya makuzi na malezi bora ya watoto wetu,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha teknolojia inayotumika katika Kiwanja hicho inalenga kuwanufaisha watoto, kuzingatia umri wao na kuendelea kukuza pamoja na kutunza mila na desturi za jamii.
Amesema Kiwanja hicho hakipaswi kuwa chanzo cha kuharibu watoto, akitoa wito wa kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanaendana na malengo ya malezi bora na ustawi wa watoto.
