Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesisitiza utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu matumizi ya Stendi ya Magufuli, akieleza kuwa uwekezaji huo wa zaidi ya Shilingi bilioni tatu unapaswa kunufaisha wananchi na kuongeza mapato ya Manispaa ya Ubungo.
Kairuki ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo, akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufuatilia suala hilo na kuhakikisha stendi inatumika ipasavyo.
Amesisitiza kuwa mabasi ya mikoani yanapaswa kutumia Stendi ya Magufuli kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili kupunguza msongamano na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
“Mimi kama Mbunge wa Kibamba, nitasimamia kila ambacho kimeelekezwa na Serikali. Nitasimamia maagizo ya Mkuu wa Mkoa,” amesema Kairuki.
Ameahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo hadi Stendi ya Magufuli itumike kikamilifu kwa manufaa ya wananchi na Manispaa ya Ubungo.
